Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, wilayani Kilombero, imeibuka mshindi wa kwanza katika Mkoa wa Morogoro kwenye Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yaliyohitimishwa Agosti 8, baada ya kuonesha ubunifu, ubora na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Jamary Idrisa Abdul, alisema ameridhishwa na ushindi huo, ambao umetokana na ushirikiano mkubwa kati ya watumishi wa halmashauri na wakulima.
Alisema siri ya mafanikio hayo ni utekelezaji wa vitendo wa shughuli za maendeleo zinazofanywa na wananchi, hali ambayo imekuwa chachu ya kuongeza ubunifu na ubora katika maonesho hayo.
"Ushindi huu unatupa hamasa kubwa. Mwaka 2027 tunajipanga kuboresha zaidi ushiriki wetu ili kuwania ubingwa wa jumla wa Maonesho ya Nane Nane," alisema Jamary.
Aliongeza kuwa halmashauri hiyo ina shamba la mfano lenye mazao mbalimbali ya kimkakati yanayolenga kukuza kilimo biashara, na kwamba itaendelea kuboresha teknolojia za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa sasa, alisema, halmashauri imejikita katika kuhamasisha kilimo cha mazao ya viungo kama pilipili manga, kakao na mdalasini, huku ikitoa miche bure kwa wananchi ili kuongeza uzalishaji na kipato.
Aidha, alisema halmashauri inaandaa ziara ya madiwani kwenda Zanzibar kujifunza zaidi kuhusu kilimo cha mazao ya viungo, ili maarifa yatakayopatikana yawasaidie kuwahamasisha wananchi kulima mazao hayo kwa wingi na kuongeza uchumi wa wilaya.
Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba lilikuwa miongoni mwa vivutio vikubwa katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki, ambapo wananchi wengi walifika kujionea mazao na teknolojia mbalimbali zilizowasilishwa.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari walipongeza ubunifu wa halmashauri hiyo na kushauri halmashauri nyingine kuiga mfano wa Mlimba kwa kuwekeza katika mazao ya kimkakati na kutoa mafunzo kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kipato.
Mwisho.









0 Comments