Na Matukio daima App Dodoma
Ng'ombe 56 waliokuwa mali ya mfugaji Clement Bernad sasa wamebaki kuwa sehemu ya historia yake ya ufugaji, ukame unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi na kupungua kwa malisho vimemlazimisha kubadili mfumo wa ufugaji, akipunguza idadi ya mifugo na kuanza kuangalia zaidi uwezo wa kuzalisha malisho na kuihudumia mifugo aliyonayo.
Bernad mkazi wa kijiji cha Mtanana wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma ni mfano wa mabadiliko yanayowakabili wafugaji katika eneo hilo, uhaba wa malisho unalazimisha mifugo kutafuta chakula nje ya maeneo ya wafugaji na wakati mwingine kuingia katika mashamba ya wakulima, hali inayochochea migogoro kati ya pande hizo mbili.
Bernad anasema baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalam kutoka Chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo ( SUA ) kuhusu ufugaji unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, ameamua kupunguza idadi ya ng'ombe wake na kubaki na idadi anayoamini anaweza kuihudumia kwa malisho na rasilimali alizonazo.
"Nilikuwa na ng'ombe 56 wa kienyeji, lakini baada ya kupata elimu nimeona umuhimu wa kuwa na mifugo ambayo ninaweza kuihudumia vizuri badala ya kuwa na mifugo mingi ambayo inakosa chakula," anasema Bernad.
Uamuzi huo unaakisi changamoto kubwa inayowakabili wafugaji nchini ambapo mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakibadilisha upatikanaji wa malisho na maji, hali inayogusa moja kwa moja uzalishaji wa mifugo ikiwemo maziwa.
Afisa Ugani wa Kata ya Mtanana Dominica Samweli Swai, anasema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa miongoni mwa sababu zinazoendelea kuchochea migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwasababau wafugaji wakikosa malisho wanalazimika kuuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Anasema suluhisho mojawapo ni kuwahamasisha wafugaji kuanza kuzalisha malisho katika maeneo yao ili kupunguza utegemezi wa malisho ya asili na ulazima wa kupeleka mifugo kutafuta chakula maeneo mengine.
"Wafugaji wengi wamehamasika kupanda malisho katika maeneo yao. Kama wafugaji watabadilika na kuacha mfumo wa kuchunga mifugo yao bila kuwa na uhakika wa malisho, tunaweza kupunguza migogoro mingi kati ya wakulima na wafugaji," anasema Swai.
Kata ya Mtanana pekee wafugaji 1,320 wenye jumla ya mifugo 7,829, idadi inayoweka wazi ukubwa wa mahitaji ya malisho katika eneo ambalo linakabiliwa na changamoto ya ukame.
Hata hivyo, kupanda malisho pekee kunaweza kusiwe jibu la muda mrefu iwapo aina ya malisho inayotumika haiwezi kustahimili vipindi virefu vya ukame.
Hapo ndipo watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameingia kazini kutafuta aina za malisho zinazoweza kustahimili ukame, huku wakilenga kutoa suluhisho linaloweza kuwasaidia wafugaji kuendelea kuzalisha mifugo hata katika mazingira yanayobadilika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungmza na waandishi wa habari Mkuu wa mradi kutoka Idara ya sayansi za wanyama, ufugaji viumbe maji na nyanda za malisho Chuo kikuu SUA, Prof. Sebastian Chenyambaga amesema utafiti huo ni sehemu ya mradi unaolenga kuimarisha uwezo wa wafugaji kustahimili na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, unaofadhiliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Mradi huo wa miaka mitatu ulianza Oktoba 2025 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2028, ukiangalia namna mabadiliko ya tabianchi yanavyowaathiri wafugaji na kutafuta mbinu zinazoweza kuongeza uwezo wao wa kukabiliana na athari hizo.
Mradi unatekelezwa katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Kishapu mkoani Shinyanga na Miatu mkoani Simiyu, maeneo ambayo yamechaguliwa katika utekelezaji wa utafiti huo.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka Idara ya sayansi za wanyama, ufugaji viumbe maji na nyanda za malisho Chuo kikuu SUA, Dkt. Doris Lutatenekwa amesema utafiti pia unaenda sambamba na kupima aina za malisho zinazostahimili ukame.
Lengo la utafiti huo si kutafuta malisho ya kuokoa mifugo pekee, bali pia kuangalia namna wafugaji wanavyoweza kuendelea kuzalisha maziwa na bidhaa nyingine za mifugo katika mazingira yenye changamoto ya ukame.
Mkurugenzi wa Costech Dkt. Amos Nungu anasema mradi huo ni miongoni mwa hatua zinazolenga kutekeleza Dira ya Tanzania ya 2050 kwa kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Anasema tafiti zinazolenga kupata suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi ni muhimu katika kujenga jamii yenye uwezo wa kustahimili mabadiliko ya mazingira na kulinda shughuli za kiuchumi za wananchi.
Kwa wafugaji kama Bernad, mabadiliko hayo hayapo tena kwenye vitabu au mijadala ya wataalamu, yameingia moja kwa moja katika maisha yao yakimlazimisha mfugaji kujiuliza si tu “nitafuga ng'ombe wangapi?”, bali pia “nitawapataje chakula wakati mvua hazitoshelezi?”











0 Comments