Header Ads Widget

BIMA YA KILIMO YATAJWA KINGA YA HASARA KWA WAKULIMA, WAFUGAJI NA WAVUVI.


NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

MWANZA

Wakulima, wafugaji na wavuvi nchini wametakiwa kutumia huduma za bima kulinda mitaji na shughuli zao za kiuchumi dhidi ya majanga mbalimbali yanayoweza kusababisha hasara.

Rai hiyo imetolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) wakati wakizungumza na waandishi wa habari , Afisa kutoka TIRA, Halfan Isango, na kueleza kuwa wamewafikia wananchi kwa  lengo la kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa bima, hususani bima zinazolenga sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Ameeleza  kuwa wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali za bima zinazowasaidia kujikinga na athari za majanga yanayoweza kutokea katika shughuli zao za uzalishaji.


Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kanda ya Ziwa, Stella Marwa, amesema NIC inatoa elimu kwa wakulima na wafugaji kuhusu umuhimu wa kuwa na bima, huku ikitoa huduma za bima ya mali na ajali pamoja na bima za maisha.

Amesema bima ya kilimo inawalinda wakulima dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo ukame, mvua zilizozidi na wadudu waharibifu, pamoja na athari nyingine zinazoweza kusababisha mavuno kuwa pungufu.

“Kwa mfano, mkulima anaweza kuwa amekuwa akivuna magunia 50 kila mwaka, lakini kutokana na janga la ukame akavuna magunia 20. Akiwa na bima inayohusisha mavuno pungufu, anaweza kufidiwa kulingana na masharti ya bima na kumsaidia kukabiliana na hasara iliyotokea,” amesema Marwa.

Stella amesema NIC pia inatoa bima kwa wavuvi, ikiwemo wanaotumia vizimba na wale wanaotumia mitumbwi, ambapo bima hizo zinawalinda dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri shughuli zao.

Aidha, amefafanua kuwa wavuvi wanaotumia vizimba wanaweza kulindwa dhidi ya majanga yanayoweza kusababisha vifo vya samaki kutokana na magonjwa au mabadiliko ya hali ya hewa katika maji, huku nyavu na injini za vyombo vya uvuvi pia zikiwa miongoni mwa mali zinazoweza kuwekewa bima.

Amesema bima za ajali kwa wavuvi pia ni muhimu, kwani endapo mvuvi atapata ajali na kupoteza maisha akiwa kazini, familia yake inaweza kupata fidia kulingana na masharti ya bima.

Hata hivyo ameleeza kuwa NIC inatoa bima kwa wafugaji wa ng’ombe wa kienyeji na kisasa, wakiwemo ng’ombe wa nyama na maziwa, dhidi ya majanga yanayoweza kusababisha hasara.

Ametaja baadhi ya majanga hayo kuwa ni uchinjaji wa lazima kutokana na ushauri wa daktari wa mifugo, ajali na kushambuliwa na wanyama au nyoka, ambapo mfugaji mwenye bima anaweza kupata fidia kulingana na mkataba wa bima.

Marwa amesisitiza kuwa bima ni muhimu pia kwa wafugaji wanaotaka kutumia mifugo yao kama dhamana ya kupata mikopo, kwa kuwa taasisi za kifedha huhitaji dhamana hiyo iwe imelindwa dhidi ya hatari mbalimbali.

“Ukiwa na bima ni rahisi kupata huduma nyingine za kifedha kama mikopo kutoka benki, lakini pia unakuwa umejikinga dhidi ya hasara,” amesema.


Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Bima ya Reliance, Monika Kijuu, amesema kampuni hiyo inaendelea kutoa huduma za bima katika sekta ya kilimo, ufugaji na ufugaji wa samaki kwa lengo la kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa kujiamini zaidi.

Amesema bima inamsaidia mkulima au mfugaji kupunguza athari za majanga yanapotokea, kwani kampuni ya bima humsaidia kurejesha sehemu ya hasara kwa mujibu wa masharti ya mkataba wa bima.

“Tunatoa huduma za kilimo na ufugaji ili kuwafanya wakulima na wafugaji waweze kufanya shughuli zao wakiwa na amani, kwa maana kwamba jambo lolote likitokea wanakuwa na uhakika wa kupata msaada kulingana na huduma waliyochukua,” amesema Kijuu.

Amesema kampuni hiyo pia inaendelea kutoa huduma zinazohusu mifugo ya kawaida pamoja na ufugaji wa samaki, huku akiwataka wakulima na wafugaji kutumia huduma hizo kulinda mitaji na uchumi wao.

Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa sekta ya bima nchini ni salama na kwamba wanapochukua huduma za bima, mamlaka na kampuni zinazohusika zina wajibu wa kuhakikisha wanapata malipo kwa wakati na kwa kiwango kinachostahili kulingana na masharti ya mkataba.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI