Header Ads Widget

TAASISI ZA ELIMU YA UFUNDI ZAHIMIZWA KUANDAA WAKUFUNZI WENYE UWEZO WA KUTUMIA AI

 








Na Matukio Daima Media, Morogoro 

TAASISI za elimu ya ufundi stadi nchini zimehimizwa kuharakisha maandalizi ya wakufunzi wenye uwezo na ujuzi wa kutumia Akili Mnemba (AI) ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa pamoja na baadaye ya soko la ajira, huku ikisisitizwa kuwa teknolojia hiyo itumike kama nyenzo ya kuboresha ufundishaji na si kuchukua nafasi ya walimu.


Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Prof. Sifuni Mchome, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Baraza la Uongozi la Tano la Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), akieleza kuwa maendeleo ya teknolojia yanahitaji taasisi za elimu kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kuitumia AI kuongeza ubora wa mafunzo.


Amesema pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya akili mnemba duniani, mwalimu bado ana nafasi kubwa katika kujenga uwezo wa mwanafunzi, hususan katika mafunzo ya vitendo, maadili na ubunifu, hivyo AI inapaswa kuonekana kama chombo cha kumsaidia mwalimu na si mbadala wake.


Prof. Mchome pia anasema Tanzania ina maelfu ya watu wenye ujuzi wa kazi mbalimbali za mikono ambao hawajatambulika rasmi katika mfumo wa kitaifa, akitolea mfano wachongaji wa vinyago, mafundi vyuma na wataalamu wengine waliopata ujuzi kupitia uzoefu.


Amesema changamoto iliyopo ni kuhakikisha ujuzi huo unatambuliwa, unapimwa na kuthibitishwa ili watu hao waweze kupata fursa zaidi za kiuchumi na kuwa sehemu ya nguvu kazi inayotambulika nchini.


Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Tano la Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), Dkt. Prosper Mgaya, amesema baraza hilo litaelekeza nguvu katika kuimarisha ubora wa mafunzo, kufanya tafiti na kuhakikisha chuo kinazalisha wakufunzi wanaoendana na mahitaji ya Taifa.


Amesema hatua hiyo inaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi unaoongozwa na maarifa, teknolojia na rasilimali watu wenye ujuzi wa vitendo.


Naye Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Uongozi la MVTTC, Prof. Eng. Zacharia Mganilwa, amesema mabadiliko ya teknolojia yanahitaji taasisi za elimu ya ufundi kuendelea kufanya maboresho ya mara kwa mara katika mitaala na mbinu za ufundishaji ili wahitimu waweze kukabiliana na ushindani wa soko la ajira.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuboresha mfumo wa mafunzo ya ufundi kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi, teknolojia na mahitaji ya soko la ajira, sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa VETA wa mwaka 2026 hadi 2031.

Amesema mafunzo ya ufundi yana nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia katika kuongeza uzalishaji na kujenga uchumi wa Taifa.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), Dkt. Andrew Boy, amesema chuo hicho kinaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia, mitaala na uwezo wa wakufunzi ili kuhakikisha kinazalisha walimu wa ufundi wenye uwezo wa kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya elimu ya amali nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI