Header Ads Widget

SELF MICROFINANCE KUWAWEZA WANANCHI KATIKA MNYORORO WA THAMANI WA KILIMO KWA KUTOA MIKOPO.

 


Na CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

TAASISI ya Self Microfinance Fund imeeleza kuwa mikopo inayotolewa kwa wananchi inalenga kuwawezesha kushiriki katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji hadi ufikishaji wa bidhaa katika masoko.

Afisa Mikopo wa Self Microfinance Fund, Adolf Itinde, ameeleza kuwa taasisi hiyo haitazami mkopo wa kilimo kwa upande wa uzalishaji pekee, bali inawawezesha wananchi wanaohusika na shughuli mbalimbali zinazounda mnyororo wa thamani, ikiwemo uchakataji, usafirishaji, uhifadhi, matumizi ya teknolojia na masoko.

Itinde ameleeza kuwa hatua hiyo inalenga kuwasaidia wananchi kuongeza tija na thamani ya bidhaa zao badala ya kuuza mazao ghafi bila kunufaika ipasavyo na fursa zilizopo katika hatua nyingine za mnyororo wa thamani.

“Tunatoa mikopo kwenye mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji, uchakataji, usafirishaji, uhifadhi, matumizi ya teknolojia hadi masoko. Hii inasaidia kuongeza thamani ya bidhaa na kuwawezesha wananchi kunufaika zaidi na shughuli zao,” amesema Itinde

Amesema Self Microfinance Fund ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha inayotoa elimu ya fedha, mikopo pamoja na huduma mbalimbali za bima, ikiwemo bima ya moto, maisha na kilimo.

Aidha amefafanua kuwa mikopo hiyo inatolewa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara, viwanda na usafirishaji, huku waombaji wakitakiwa kuwa Watanzania wanaofanya shughuli halali nchini

Itinde amesema miongoni mwa vigezo vya kupata mkopo ni mwombaji kuwa na biashara ambayo imefanya kazi kwa angalau miezi 12, kuwa na historia nzuri ya ukopaji na urejeshaji pamoja na kuwa na dhamana inayokubalika.

Amesema taasisi hiyo pia huwapatia waombaji elimu ya fedha na mikopo kabla ya kuwawezesha, ili kuhakikisha wanaelewa namna ya kutumia fedha hizo kwa tija na kutimiza wajibu wa marejesho.

Akizungumzia fursa zilizopo katika ufugaji, Itinde amesema soko la Mwanza lina mahitaji ya kuku na mayai, hivyo wafugaji wenye kuanzia kuku 100 wanaweza kufika katika ofisi za taasisi hiyo kupata elimu na kuomba mikopo baada ya kukidhi vigezo.

Aidha, amesema taasisi hiyo yenye matawi 12 nchini inatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 50 katika mwaka huu wa fedha, huku Tawi la Mwanza likilenga kutoa zaidi ya Sh bilioni 8.

Amesema uwezeshaji huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa 2050 ya kujenga uchumi unaozalisha, unaoshirikisha wananchi na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Itinde amewahimiza wananchi, hususan wanaojihusisha na kilimo, ufugaji na biashara, kutumia fursa za elimu ya fedha, mikopo na bima zinazotolewa na Self Microfinance Fund ili kukuza shughuli zao na kuongeza kipato.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI