Header Ads Widget

RC KHERI JAMES APONGEZA UWEKEZAJI GOLDEN GLOW HOTEL

 

TAZAMA TUKIO ZIMA LIVE BONYEZA LINK HII

NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,IRINGA 

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amepongeza uwekezaji wa Golden Glow Hotel iliyopo eneo la Kihodombi, Kata ya Isakalilo, Manispaa ya Iringa, akisema uwekezaji huo utasaidia kukuza sekta ya utalii na uchumi wa mkoa huo.

Kheri James aliyasema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa hoteli hiyo, akieleza kuwa uwepo wa huduma bora za malazi ni muhimu katika kuwafanya watalii na wageni wanaofika Iringa kubaki kwa muda mrefu badala ya kwenda mikoa ya jirani kutafuta huduma hizo.

Alisema Iringa ina vivutio vingi vya utalii na fursa mbalimbali za kiuchumi, hivyo ni muhimu kuendelea kuwekeza katika hoteli, usafiri na huduma nyingine zinazohusiana na utalii.

“Uwekezaji huu ni muhimu kwa sababu unawafanya watalii wanapofika Iringa kuwa na sehemu nzuri ya kukaa na hivyo kuongeza uwezekano wa kuendelea kubaki hapa badala ya kwenda mikoa ya jirani kutafuta hoteli za kulala,” alisema.


Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Wairinga wanaoishi nje ya mkoa huo kurejea na kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika maeneo mbalimbali, akisisitiza kuwa maendeleo ya mkoa yanahitaji ushiriki wa wananchi wenyewe.

Alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, hivyo wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hizo badala ya kusubiri wawekezaji kutoka nje pekee.


“Ni jukumu la wananchi wa Mkoa wa Iringa kuchangamkia fursa zilizopo na kuwekeza. Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hizo kwa maendeleo yao binafsi na maendeleo ya mkoa kwa ujumla,” alisema.

Kheri James pia alitaja kukamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Iringa kuwa fursa kubwa kwa wananchi na wafanyabiashara, akisema jengo la abiria liko katika hatua za mwisho za kukamilika.

Alisema uwanja huo unaweza kuongeza idadi ya watalii, wafanyabiashara na wawekezaji wanaofika Iringa, jambo litakaloongeza mahitaji ya huduma mbalimbali.

Aliwataka wananchi kuanza kujiandaa kutumia fursa hizo kwa kuwekeza katika hoteli, migahawa, usafirishaji, utalii, nyumba za kulala wageni na huduma nyingine.

“Fursa kubwa kwa sasa ni kukamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Iringa.

 Jengo la abiria lipo mbioni kukamilika, hivyo ni wajibu wa wananchi wa Mkoa wa Iringa kuchangamkia fursa hii Tukichelewa, wageni watachangamkia fursa hizo,” alisema.

Aidha, alisema uwekezaji katika sekta ya hoteli ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utalii mkoani humo, huku akisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kutumia vizuri fursa za kiuchumi.

Kheri James alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hizo kujenga uchumi wa familia, jamii na taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Golden Glow Hotel, Ernest Mtavilalo, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kuzindua hoteli hiyo.

Mtavilalo alisema uzinduzi huo una maana kubwa kwake na kwa familia yake, akieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo ni matokeo ya safari iliyohitaji uvumilivu, ushauri, upendo na ushirikiano.

“Namshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika katika siku hii muhimu ya uzinduzi wa Golden Glow Hotel

 Ni siku ambayo kwangu na kwa familia yangu ina maana kubwa sana,” alisema.

Alitoa shukrani maalumu kwa familia yake, hususan mke wake pamoja na kaka yake, kwa kusimama naye katika safari hiyo.

“Ninapenda kuishukuru familia yangu, hasa mke wangu pamoja na kaka yangu, kwa kusimama nami katika safari hii. 

Safari hii haikuwa rahisi, lakini upendo, ushauri, uvumilivu na msaada wenu umekuwa sehemu kubwa ya kufanikisha ndoto hii,” alisema.

Pia aliwashukuru mafundi, wahandisi na wote walioshiriki katika ujenzi na maandalizi ya hoteli hiyo, akisema kila mmoja ameacha alama katika kufanikisha mradi huo.

Mtavilalo alisema Golden Glow Hotel kwake si jengo pekee, bali ni ndoto iliyogeuka kuwa uhalisia pamoja na ahadi ya kutoa ajira na kuchangia maendeleo ya jamii ya Iringa.

“Kwangu Golden Glow si jengo tu, ni ndoto iliyoigeuka kuwa uhalisia na ni ahadi yetu ya kutoa ajira na kuchangia maendeleo ya jamii yetu hapa Iringa,” alisema.

Alisema hoteli hiyo inalenga kutoa huduma kwa wageni wanaofika Iringa na kushiriki katika kukuza shughuli za kiuchumi ndani ya mkoa huo.

Mtavilalo alihitimisha kwa kuwashukuru viongozi, wageni waalikwa, ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria hafla hiyo, akisema uwepo wao umeifanya siku hiyo kuwa ya kipekee.

Mkuu wa wilaya ya Iringa Banjamin Sitta alisema kuwa uzinduzi wa Golden Glow Hotel unaongeza uwekezaji katika sekta ya ukarimu wilaya hiyo  na unatoa fursa zaidi za ajira na huduma kwa wageni, huku ukiweka msisitizo wa umuhimu wa wananchi kutumia fursa za uwekezaji zinazojitokeza kutokana na ukuaji wa utalii na miundombinu ya mkoa huo.

PICHA ZOTE TAZAMA HAPA CHINI⬇️⬇️⬇️

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI