NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MKUU wa wilaya ya Moshi, Kisare Makori amesitisha shughuli zote za mwekezaji katika Shamba la chama cha msingi cha Kirima Boro na Kimasio katika eneo la Sangiti kwa siku thelathini baada ya Serikali kujiridhisha kuwa Mwekezaji huyo hakufuata utaratibu wa kumiliki eneo hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu huyo wa wilaya akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama pamoja na Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi kufanya ziara katika kata ya Kibosho Kirima na kufanya Mkutano wa hadhara.
Hatua ya kusimamishwa kwa Mwekezaji huyo ilipokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi walioshiriki mkutano huo.
Katika mkutano huo Mkuu wa wilaya alikuwa anatekeleza majukumu yake ya kusikiliza kero za wananchi na kutoa jibu la kero za mwekezaji katika shamba la Sangiti na ile ya upotevu wa mbao katika Kata ya Kibosho Kirima.
Katika mkutano huo, mwananchi mmoja alimweleza Mkuu wa wilaya kwamba pamoja na kwamba Mwenyekiti na Katibu wa KIMASIO AMCOS kuwa na kesi mahakamani inayohusu matumizi mabaya ya madaraka kuwekeza kwenye shamba hilo, bado wako ofisini wakitekeleza majukumu yao jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
Mkuu wa Wilaya alimwelekeza Afisa Ushirika wa Wilaya kuwasimamisha viongozi hao kwa barua na kumpa nakala ifikapo Septemba 22 mwaka huu.
Kuhusu tuhuma za wizi wa mbao, wananchi walielezwa kuwa TAKUKURU wanafanya uchunguzi na bado haujakamiika.
Wananchi walimweleza kero mbalimbali zilizohusu barabara, upatikanaji wa maji, umeme, umiliki wa maeneo katika shamba la Sangiti na ANTIPI, kero za TASAF, ukosefu wa vyoo na madawati katika shule za msingi na ukosefu wa maabara katika shule ya Sekondari Masoka na kero hizi zilipata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu na nyingine Mkuu wa wilaya alizibeba ili wakazifanyie kazi.
Katika mkutano huo Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi alimshukuru sana Mkuu wa Wilaya na wataalamu wake kwa jinsi wanavyowahudumia wananchi katika Wilaya ya Moshi.
Mkuu wa wilaya alimshukuru na kumpongeza Mbunge kwa jinsi anavyopambania Wanajimbo ikiwa ni pamoja na wananchi wa Kata ya Kibosho Kirima na kuwataka wananchi kuchapa kazi pamoja na kuwaombea viongozi wanaowaongoza ili maendeleo yaweze kuonenakana katika jamii zao.
Mwisho.
0 Comments