NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi alitembelea Kata ya Arusha Chini akiambatana na wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Mbunge na jopo la wataalamu walikwenda kuangalia eneo ambalo wakulima wa Kata ya Arusha Chini wanatamani kujengewa skimu ya umwagiliaji kwani wana eneo kubwa na maji ya kutosha kumwagilia.
Kwa upande wa Tume ya umwagiliaji, Mbunge aliambatana na Mhandisi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wa Mkoa wa Kilimanjaro Jacob Towa pamoja na Wahandisi wa Wilaya ya Moshi, Elikia Mponji na Mhale Tsere Nakei.
Mbunge na ujumbe wake walipokelewa na viongozi mbalimbali wa Kata ya Arusha Chini akiwemo Leonard Waziri (diwani), pamoja na viongozi mbalimbali wa Vijiji vya Mikocheni na Chemchem.
Vilevile walikuwepo viongozi na wajumbe wa Chama Cha Umoja wa Wamwagiliaji (CHEMIKO).
Akiwakaribisha wataalamu, Diwani alieleza kuwa wakulima wa Arusha Chini wanalo eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari elfu nne (4000) ambalo linafaa kujengewa skimu ya umwagiliaji ambapo mazao yanayolimwa mara tatu kwa mwaka ni pamoja na mahindi, maharage, nyanya, mpunga, mbogamboga na matikiti maji.
Wataalamu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji walijionea eneo linalolimwa, na vyanzo vya maji na kujiridhisha kwamba, ikiwa fedha zitapatikana, eneo hili kutajengwa mradi mkubwa sana wa umwagiliaji.
Mbunge amewaambia viongozi hao wa Kata kuwa ataiomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kujenga Skimu kubwa na ya kisasa katika Vijiji hivyo na kuleta tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na biashara kwani ni hitaji lao kubwa kwa hivi sasa.
Mwisho..
0 Comments