Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Makamu wa Rais Dkt. Philipo Mpango ametaka wazazi kuhakikisha wanapeleka shule watoto wao na kuhakikisha watoto hao wanamaliza masomo yao.
Dk.Mpango alisema hayo akiwa wilayani Buhigwe mkoani Kigoma ambapo alifungua madarasa matatu na ofisi mbili za walimu katika shule ya Msingi Muyama yaliyokarabatiwa na Tanzania Commercial Bank.
Katika wito wake kwa wananchi wa mkoa Kigoma Makamu wa Rais amekemea tabia ya wazazi kuwaoza watoto wa kike mapema na badala yake ametaka waache wamalize masomo yao na kupata elimu ambayo itawafanya kuwa viongozi au watendaji kusaidia maendeleo ya nchi na jamii zao huku akitaka watoto wenye ulemavu kupewa nafasi ya kupata masomo.
Makamu Rais alisema kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye miundo mbinu ya shule kwa ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na kuongeza idadi kubwa ya walimu hivyo alisema kuwa lazima wazazi wahakikishe watoto wanasoma na kumaliza elimu yao na kwa sasa serikali inaendesha program ya kutoa elimu yenye ujuzi hivyo watoto waache wasome ili elimu iwasaidie baadaye.
Akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Commercial Bank, Sabasaba Moshingi alisema kuwa benki hiyo imetumia kiasi cha shilingi milioni 78 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa matatu, ofisi mbili za walimu, madawati 25 na mashine ya kurudufia karatasi.
Moshingi alisema kuwa fedha hizo ni sehemu ya kiasi cha shilingi milioni 300 ambazo Benki hiyo imetoa kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kurudisha kwa jamii na kubainisha kwamba mazingira mazuri ya uendeshaji shughuli za benki yaliyowekwa na serikali imewezesha benki kuongeza mtaji na kufikia kiasi cha shilingi trilioni 1.3.
0 Comments