Na Matukio Daima Media, Iringa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa likiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), Allan Bukumbi, limefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Mlima Nyang’oro na kuendesha zoezi la upigaji kura za siri kwa lengo la kuwabaini wahalifu wanaohusika na kurusha mawe kwenye magari.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ongezeko la vitendo vya uhalifu katika eneo la mlima huo, ambapo baadhi ya watu wasiojulikana wamekuwa wakirusha mawe kwenye magari yanayopita, hali inayohatarisha maisha ya abiria na kusababisha uharibifu wa mali.
Akizungumza katika mkutano huo, RPC Bukumbi amesema ushiriki wa wananchi katika kutoa taarifa ni muhimu katika kuhakikisha amani na usalama vinarejea katika eneo hilo.
“Katika jamii yetu yapo matukio yanayoendelea hasa kwa watoto, na niwaombe wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wao hawazururi usiku. Wakifika nyumbani kutoka shule, wabaki majumbani kwa ajili ya usalama wao. Malezi ni jukumu la msingi kwa mzazi,” alisema RPC Bukumbi.
RPC Iringa akiwa eneo la tukio ambalo magari yalikuwa yakipigwa mawe.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi limeanzisha programu maalum ya kukamata watoto wanaozurura nyakati za usiku.
“Tutaanza kuwakamata watoto wa umri mdogo wanaotembea usiku. Tukiwakamata, tutawaambia watupeleke kwa wazazi wao na tuchukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema.
kamanda wa polisi mkoa wa Iringa (RPC) Allan Bukumbi akimpa maelekezo mkuu wa polisi wilaya ya Iringa (OCD) Bernad Samala (kushoto) kuendesha zoezi la kura za siri kufichua wahalifu milima Nyang'oro wakati wa mkutano wa hadhara picha na Matukio Daima Media
Kamanda Bukumbi pia alizungumza na watoto waliokuwepo kwenye mkutano, akiwashauri waepuke tabia ya kuzurura na badala yake watumie muda wao kujisomea na kuwa nyumbani baada ya shule.
Aliwahimiza wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini viashiria vya uhalifu ili kusaidia Jeshi la Polisi kuimarisha usalama wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Iringa (OCD), Bernad Samala alisema:
“Jeshi la Polisi haliwezi kufanya kazi pekee bila ushirikiano wa wananchi. Matukio haya ya kihalifu yanaweza kudhibitiwa iwapo kutakuwa na mshikamano kati ya polisi na jamii.”
Wananchi wa eneo hilo walielezea changamoto mbalimbali wanazokutana nazo, huku wakisisitiza umuhimu wa polisi kulinda usiri wa wanaotoa taarifa za uhalifu ili kuhakikisha usalama wao.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Gasper Kihongo, alisema:
“Uhalifu unaofanyika hapa mara nyingi unafanywa na watu kutoka maeneo ya mbali, siyo wenyeji wa kijiji. Hali hii inachafua jina la kijiji chetu.”
Naye mfugaji Bernard Ilomo aliongeza kuwa wizi bado ni tatizo kubwa katika kata yao.
“Jeshi la Polisi linapaswa kuingilia kati haraka. Pia wapo baadhi ya askari wasiotoa ushirikiano; hata ukitoa taarifa hawazifuatilii,” alisema Ilomo.
0 Comments