Na Amon Mtega,Namtumbo
MKURUGENZI mtendaji Aleksandra Ryabchenko wa kampuni ya Mantra Tanzania Limited inayojishughulisha na madini ya Urani katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ameahidi kupitia kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na jamii katika kufanikisha miradi mbali mbali kwenye jamii ya Mkoani humo ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuinua kiuchumi.
Ryabchenko ametoa ahadi hiyo wakati akikabidhi msaada wa mashine za maabara zinazotambulika kwa jina la Chemical Analyzer zenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni thelathini (Tsh,30,000,000=) ambazo zitatumika katika Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo.
Mkurugenzi huyo akikabidhi msaada wa mashine hizo kwenye Hospitali hiyo kupitia mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya katika ofisi ya Wilaya hiyo amesema kuwa kampuni ya Mantra Tanzania tangu ilipoanza shughuli za madini ya Urani kwenye Wilaya hiyo kampuni hiyo imekuwa ikishilikiana na jamii hasa ya Wilaya ya Namtumbo katika kutekeleza miradi mbalimbali kwenye jamii .
Amefafanua kuwa malengo kipindi cha miaka mitano 2023 hadi 2028 kampuni imejipanga kikamilifu kuendelea kuwekeza kwenye miradi ambayo jamii itanufaika nayo na kuifanya jamii iweze kusongambele kiuchumi .
Mkurugenzi huyo amesema kuwa licha ya kuweka mpango wa miaka mitano mbele ya namna ya kuisaidia jamii lakini kampuni hiyo imeshafanya mambo mengi kwa kushirikiana na wanajamii kama ujenzi wa maktaba za kisasa kwenye baadhi ya shule za Sekondari, Upatikanaji wa maji kwenye baadhi ya taasisi za umma kwenye baadhi ya shule na sehemu za Afya , uchangiaji wa ujenzi wa ofisi za Serikali kwa baadhi Vijiji , Kuviwezesha baadhi ya vikundi vya kijamii katika utunzaji wa mazingira kwa kuotesha miti asili na matunda,lakini pia na utoaji wa Elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule zilizopo maeneo ya barabara.
Aidha kampuni hiyo imesaidia kutoa vifaa mbalimbali vya Elimu kwa wanafunzi wa makundi maalumu yaani vitabu nundu ,fimbo za kutembelea pamoja na baiskel (Wheelchair)kwa baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wa kutokutembea.
Hata hivyo ameelezea kufuatia utekelezaji wa mradi wa madini ya Urani kuwa utaanza kabla ya mwisho wa mwaka huu 2023 na kuwa taratibu zote kwa asilimia kubwa zimeshafanyika ikiwemo upatikanaji wa vibali mbalimbali na Leseni.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya akipokea mashine za maabara kwa matumizi ya Hospitali ya Wilaya hiyo amesema kuwa ni ukweli usiyopingika kampuni ya Mantra Tanzania Limited imekuwa ikifanya kazi za kijamii licha ya kuwa kampuni hiyo haijaanza kufanya kazi ya madini ya Urani .
Malenya ameipongeza kampuni hiyo na kuwa mashine walizopewa zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili wakazi wa Wilaya hiyo wapatiwe huduma ya Afya iliyobora kama Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo Afya .
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Rabani Thomas amesema anatamani kampuni hiyo ianze shughuli za madini ya Urani mara moja ili kuongeza uchumi ndani ya Mkoa na Taifa kwa ujumla
0 Comments