Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WADAU wa elimu katika wilaya ya Kigoma wameitaka serikali kupitia halmashauri kuweka sheria ndogo zitakazowabana wazazi wanaoshindwa kutekeleza mpango wa chakula shuleni kwa wananfunzi.
Wito huo wa wadau umeibuliwa katika kikao cha wakuu wa shule za msingi na sekondari, wenyeviti wa bodi za shule, waratibu elimu kata na watendaji wa kata kilichotishwa na Mku wa wilaya Kigoma kuweka mkakati wa kuinua taalima shuleni.
Akizungumzia katika kikao hicho Mkuu wa shule ya Bishop Mlola, Aliamulika Kyungai alisema kuwa serikali inapaswa kuweka sheria na taratibu zitakazowabana wazazi kuhakikisha wanatekeleza mpango wa wanafunzi kula shuleni kwani chakula kina mahusiano makubwa na ufaulu mzuri kwa wanafunzi hasa wakati huu ambao wanafunzi wanasoma masomo ya ziada na kushinda shuleni hadi jioni.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kikungu Manispaa ya Kigoma Ujiji, Isidori Philipo alisema kuwa serikali imetoa maelekezo ya wazazi kuchangia chakula ili watoto wawepo shuleni hadi jioni kwa masomo ya ziada lakini baadhi ya wazazi wanakwamisha hilo na shule hazina mamlaka kisheria kuchukua hatua kwa wazazi hao.
Akichangia kwenye suala hilo wake Afisa Elimu Sekondari wa halmashauri ya wilaya kigoma, Exavery Ntambala alisema kuwa kushindwa kutekelezwa kwa agizo la serikali la wanafunzi kula shuleni linatokana na wazazi kuwa na dhana kuchangia fedha au chakula kwa ajili ya wanafunzi inawanufaisha walimu badala ya wanafunzi hivyo ametaka sheria ndogo iwekwe kuwabana wazazi.
Kwa upande wake Afisa elimu shule ya msingi manispaa ya Kigoma Ujiji, Richard Mtauka alisema kuwa wamekuwa wakitoa maelekezo ya serikali kwa shule kusimamia mipango mbalimbali ya kusimamia taaluma ikiwemo utoaji wa chakula shuleni lakini bado kumekuwa na changamoto ya utekelezaji wa mambo hayo.
Mtauka alisema kuwa kati ya shule za msingi 45 zilizopo kwenye manispaa hiyo ni shule 30 zimeanza kutoa chakula huku kukiwa na changamoto kwa baadhi ya wazazi kushindwa kutekeleza hilo huku shule 15 zikiwa hazijaanza kutekeleza mpango huo kabisa.
Akizungumza na wadau wa elimu katika mkutano huo MKUU wa wilaya Kigoma Salum Kalli amezataka kamati za uendeshaji wa shule,waratibu elimu kata na watendaji wa kata kuweka mipango mikakati ya kuinua elimu katika wilaya hiyo ikiwemo kusimamia mpango wa chakula shuleni unaotekelezeka.
Kalli alisema uwepo wa chakula shuleni una uhusiano mkubwa na kufanya vizuri kitaaluma kwa wanafunzi na kwamba serikali imetoa maelekezo ya kuwepo kwa chakula shuleni baada ya kufanya utafiti unaobainisha kuwa kuwepo kwa masomo ya ziada baada ya chakula cha mchana kwa wanafunzi kunasaidia katika kuinua taaluma na wanafunzi kushika masomo wanayofundishwa.
0 Comments