Header Ads Widget

ZAIDI YA MABASI 150 YA MOFAT YAKOSA ENEO LA KUTOLEA HUDUMA


Na Matukio DaimaApp, Dar

Imeelezwa kuwa zaidi ya mabasi 150 yaendayo haraka ya kampuni ya Mofat yamepaki kwa miezi sita sasa tangu kununuliwa kwa kukosa eneo la kutolea huduma, huku mabasi 50 pekee ndio yanayofanya kazi na kutoa huduma kwa abiria .

Akizungumza mbele ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufanya ziara,  Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE) David Kafulila amesema wamebaini changamoto kadhaa ikiwemo mabasi 150 kukosa eneo la kutolea huduma. 

Kafulila amesema ziara hiyo imelenga kukagua mradi wa mabasi yaendayo haraka unaoendeshwa kwa ubia kati ya DART na kampuni ya Mofat, ili kutathmini utekelezaji wake na kubaini changamoto zilizopo, ambapo wamebaini mabasi hayo kukosa eneo la kutolea huduma.

Amesema kuwa, kwa mujibu wa sheria, miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi inapaswa kufuatiliwa na Serikali kuanzia hatua za awali hadi mwisho wake ili kuhakikisha uwekezaji unakuwa endelevu.




“Tumefanya ziara hii pamoja na wadau wa sekta binafsi ili kuona namna mradi huu unavyoendeshwa na kubaini changamoto zake. Tumegundua kuwa zaidi ya mabasi 150 yamekaa bila kutoa huduma kwa zaidi ya nusu mwaka, jambo linalosababisha hasara kwa mwekezaji,” amesema Kafulila.

Hata hivyo, kampuni hiyo ameishsuri kuandaa ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mradi kwa kipindi cha miezi sita, ambayo itawasilishwa Serikalini kupitia kamati za juu za usimamizi wa miradi ya ubia ili kusaidia kufanyiwa maboresho na kutatua changamoto zilizopo.

Kwa upande wake, Msemaji wa kampuni ya Mofat, Philip Changala, amesema mradi huo ni wa kimkakati kwa manufaa ya Watanzania, hasa kwa wakazi wa Dar es salaam  maeneo ya Mbagala, Kivukoni na Gerezani.

Aidha aibainisha kuwa TPSF imekuwa na mchango mkubwa katika kuwasilisha changamoto za sekta binafsi Serikalini na kusaidia kupatikana kwa mrejesho.

“Tunatambua kuwa mahitaji ya usafiri ni makubwa na yanatofautiana kwa wananchi, tunaendelea kubuni huduma mbalimbali ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuhakikisha kila mmoja ananufaika na huduma zetu,” amesema Changala

Chingala ameeleza kuwa ziara ya PPP-CENTRE imekuwa chachu kwa kampuni hiyo, kwani imeonesha dhamira ya Serikali ya kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji binafsi ili kuboresha mazingira ya biashara.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI