NA MATUKIO DAIMA MEDIA
.Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Baraka Kimata, ametoa maoni yake kuhusu mwenendo wa siasa nchini, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa viongozi, uchambuzi wa kina wa misimamo ya wanasiasa na wananchi kuwa makini katika kuwachagua viongozi wao.
Akizungumza katika mahojiano,na Matukio Daima Media, Kimata alisema kuwa msamaha katika siasa si jambo la papo kwa papo bali ni mchakato unaohitaji muda, tafakuri na kuzingatia athari za matukio yaliyotokea katika jamii.
Alieleza kuwa baadhi ya matukio ya kisiasa yanaacha alama kubwa kwa wananchi na hivyo hayawezi kufutika kwa kauli za haraka bila kujenga mazingira ya maridhiano ya kweli.
“Kuomba msamaha ni neno dogo, lakini kusamehewa ni mchakato. Kuna mambo ambayo yanahitaji muda wa kuyatafakari kabla ya jamii kukubali maridhiano,” alisema.
Kimata pia alizungumzia mwenendo wa wanasiasa wanaobadilisha vyama, akisema wananchi wanapaswa kuchunguza kwa makini historia na matendo ya viongozi kabla ya kuwaamini.
Alisema kuwa baadhi ya wanasiasa hutanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya taifa, jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Tukiendelea na siasa za maslahi binafsi na kauli zisizo na tafakuri ya kina, tunaweza kulipeleka taifa mahali pabaya,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa wananchi wanapaswa kuwachunguza viongozi wanaodai kupigania haki kwa kuangalia historia yao ya uongozi na matendo yao ya nyuma badala ya maneno pekee.
Kimata alisisitiza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kuwa na malengo ya msingi ya kushika madaraka na kushiriki katika maamuzi ya kitaifa kupitia nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.
Aliongeza kuwa uimara wa chama cha siasa hupimwa kwa uwezo wake wa kuaminiwa na wananchi na kutekeleza sera zake kwa ufanisi.
Kuhusu hoja za uhamaji wa viongozi wa kisiasa, Kimata alisema kuwa ni muhimu kwa wananchi kuchambua kwa kina sababu za wanasiasa kuhama vyama na kuelewa historia yao ya kisiasa kabla ya kutoa maamuzi.
Alimtaja aliyewahi kuwa kada wa CHADEMA Mchungaji Peter Msigwa na baadaye kuhamia CCM, akieleza kuwa alishika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ubunge na nafasi za juu ndani ya chama chake cha zamani, akisema viongozi wenye uzoefu mkubwa wanapaswa kutumia maarifa yao kwa manufaa ya taifa.
Aidha, alieleza kuwa uzoefu unaopatikana katika nafasi za uongozi unapaswa kutumika kwa hekima, vinginevyo unaweza kuleta maamuzi yanayoweza kuathiri taswira ya mwanasiasa na taasisi husika.
Kimata pia alionya kuwa siasa za kubadilisha misimamo mara kwa mara zinaweza kuwachanganya wananchi na kudhoofisha imani kwa viongozi wa kisiasa.
Alitolea mfano wa matukio ya kisiasa katika baadhi ya nchi za Afrika zilizokumbwa na migogoro, akisema kuwa Tanzania inapaswa kujifunza umuhimu wa mazungumzo, maridhiano na kuweka maslahi ya taifa mbele.
Kwa mujibu wake, viongozi wanapaswa kutumia majukwaa yao ya kisiasa kujenga hoja za maendeleo badala ya kuendeleza migogoro isiyo na tija kwa wananchi.
Kimata alisisitiza kuwa watanzania wanapaswa kuwa macho na kuchambua kwa kina matendo ya viongozi wao ili kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha nchi inaendelea katika misingi ya amani na maendeleo.







0 Comments