Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
KATIBU Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Dodoma, Alexander Mallya, ametoa wito kwa wafanyabiashara nchini kuacha tabia ya kukwepa kodi na badala yake kulipa kodi kwa hiari kwani ulipaji kodi kwa hiari ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya taifa.
Akizungumza jana jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa jumuiya hiyo katika kuchochea maendeleo kupitia kodi, Mallya amesema kuwa licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wafanyabiashara, wachache wao ndiyo wanaolipa kodi ipasavyo huku wengi wakijihusisha na ukwepaji kodi.
“Ni wazi kwamba wafanyabiashara ni wengi, lakini idadi ya wanaolipa kodi ni ndogo hili ni tatizo tunalopaswa kulikemea kwa nguvu zote hivyo Tunawahamasisha wafanyabiashara wenzetu kulipa kodi kwa hiari kwa sababu ndiyo msingi wa maendeleo yetu,” amesema Mallya.
Aidha amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeanzisha Dawati la Uwezeshaji Biashara, ambalo linalenga kuwawezesha wafanyabiashara kwa kuwapatia mikopo na kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kikodi.
“Kupitia dawati hili, wafanyabiashara wataweza kupata mikopo, kuondolewa baadhi ya vikwazo, pamoja na kusaidiwa katika masuala ya usajili na ulipaji wa kodi,” amefafanua.
Kwa mujibu wa Mallya, jumla ya kero 119 za kikodi ziliripotiwa kutoka kwa wafanyabiashara, lakini juhudi za pamoja kati ya TRA na wadau wa biashara zimefanikisha kupunguzwa kwa kero hizo hadi kufikia kero 18 tu za msingi, huku nyingine zikiwa katika hatua ya kushughulikiwa.
Aidha, Mallya alipongeza Serikali kwa miradi mikubwa ya maendeleo inayotokana na kodi za watanzania ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ambayo amesema imekuwa mkombozi kwa wafanyabiashara katika usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi kwa urahisi na gharama nafuu.
Katika kuhakikisha mazingira bora ya biashara, alisema Baraza la Biashara Mkoa wa Dodoma limependekeza ufungaji wa kamera katika maeneo ya katikati ya jiji ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla na hatua hiyo ipo kwenye mchakato
“Tunaipongeza Serikali na uongozi wa Rais Samia kwa kuboresha mahusiano kati ya TRA na wafanyabiashara Zamani walikuwa wakifungiwa maduka ghafla, lakini sasa kila kitu kinazungumzika na mchakato wa kodi unafanyika kwa usawa na uelewa,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Dodoma, Gilbert Chuwa, amesema ipo haja ya Serikali kupitia TRA kuendelea kutoa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya kodi kwa wafanyabiashara ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao bila hofu wala kutoelewa sheria.
“Elimu ya kodi bado inahitajika sana. Wapo wafanyabiashara wanaokwepa kodi si kwa sababu ya nia mbaya, bali kwa kukosa maarifa sahihi kuhusu utaratibu wa kulipa kodi,” amesema Chuwa.
Naye mfanyabiashara maarufu jijini Dodoma, Sylivano James Chami, alisema hali ya biashara imeboreshwa kwa kiasi kikubwa tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani, akisisitiza kuwa kwa sasa hakuna hofu wala mazingira ya kufungiwa maduka kama ilivyokuwa hapo awali.
“Kwakweli hali imebadilika sana zamani tulikuwa tunafungiwa maduka bila hata kupewa nafasi ya kueleza lakini sasa TRA wamekuwa wasikivu na wanatoa nafasi ya mazungumzo kabla ya hatua yoyote tunaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuweka mazingira rafiki ya biashara,” amesema Chami.
Hata hivyo Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Dodoma imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha mapato ya ndani yanaimarika kupitia ulipaji sahihi wa kodi, ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuijenga Tanzania mpya.
Mwisho


.jpeg)





0 Comments