Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
MKOA wa Dodoma umeendelea kung’ara kitaifa katika sekta ya elimu baada ya kudhibiti kwa kiwango kikubwa tatizo la utoro wa walimu na wanafunzi, hatua iliyochochea ongezeko la ufaulu katika mitihani ya kitaifa.
Akizungumza Mei 6, 2026 katika mkutano wa wadau wa elimu mkoani hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, alisema nidhamu ya mahudhurio imekuwa mhimili muhimu wa mafanikio hayo.
Amesema kupungua kwa utoro kumeongeza muda wa kujifunza darasani, hali iliyosaidia walimu kukamilisha mtaala kwa wakati na wanafunzi kuelewa masomo kwa ufanisi zaidi.
“Ni muhimu kuhakikisha walimu na wanafunzi wanahudhuria kikamilifu. Hapo ndipo msingi wa ufaulu unapojengwa,” amesema.
Ameeleza kuwa, ufaulu wa darasa la saba umeongezeka kutoka asilimia 87.89 mwaka 2024 hadi 93.23 mwaka 2025, huku darasa la nne ukipanda kutoka asilimia 94.64 hadi 95.99.
Katika ngazi ya sekondari, kidato cha pili kimeonyesha ongezeko kubwa zaidi la ufaulu kutoka asilimia 86.12 hadi 98.05, hatua inayotajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na kupungua kwa utoro.
Aidha, kidato cha nne kimeongezeka kutoka asilimia 92.81 hadi 94.49, huku kidato cha sita kikiendelea kuwa na ufaulu wa juu zaidi wa asilimia 99.87 mwaka 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi thabiti wa mikakati ya elimu pamoja na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Amesema mkoa huo sasa umeshika nafasi ya pili kitaifa mwaka 2025, tofauti na miaka ya nyuma ambapo haukuwa hata katika kumi bora kwa muda mrefu.
“Msingi mkubwa ulikuwa ni kusimamia utekelezaji wa mipango yetu, ikiwemo kupambana na utoro kwa vitendo,” amesema Senyamule
Aliongeza kuwa " Juhudi hizo zimehusisha viongozi wa elimu, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla, hali iliyosaidia kuhakikisha wanafunzi wanabaki shuleni na kushiriki kikamilifu katika masomo, " Amesema.
Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu na kuweka msisitizo wa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana, huku udhibiti wa utoro ukiendelea kuwa ajenda muhimu katika kuboresha ubora wa elimu nchini.









0 Comments