Header Ads Widget

CCM YAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUUNDA TUME YA UCHUNGUZI, YAUNGA MKONO RIPOTI NA KUSISITIZA MARIDHIANO

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Mwenyekiti wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuunda tume ya uchunguzi wa matukio ya ghasia yaliyotokea Oktoba 29, 2025, kikieleza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya kulinda haki, uwazi na mshikamano wa taifa.


Akizungumza na waandishi wa habari Mei 4, 2026 jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi, Kenani Kihongosi, alisema uamuzi wa Rais kuunda tume hiyo kwa mujibu wa sheria za nchi, ikiwemo sura ya 32 ya sheria za Tanzania, ni kielelezo cha uongozi makini unaojali mustakabali wa taifa.


Ameeleza kuwa CCM imeipokea ripoti ya tume hiyo kwa uzito mkubwa, ikitambua mchango wake katika kulinda mshikamano wa taifa na kujenga msingi imara kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


 Aliongeza kuwa moja ya malengo makuu ya tume hiyo ilikuwa kusaidia taifa kujifunza kutokana na matukio yaliyotokea pamoja na kuimarisha umoja wa kitaifa, jambo ambalo chama kinatilia mkazo mkubwa.


Aidha, chama hicho kilisifu utendaji wa tume hiyo iliyokuwa chini ya mwenyekiti wake, Mohamed Othman Chande, kikieleza kuwa imefanya kazi kwa uhuru, weledi na uzalendo wa hali ya juu.


 Pongezi hizo pia zilienda kwa wajumbe wote wa tume kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.


CCM pia iliwashukuru Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni na ushahidi wao kwa utulivu na ushirikiano mkubwa wakati wa zoezi la ukusanyaji wa taarifa, jambo lililochangia kukamilika kwa kazi ya tume hiyo kwa mafanikio.


Kuhusu mapendekezo yaliyotolewa, CCM imeeleza kuyaunga mkono kikamilifu na kumshukuru Rais Samia kwa kuyapokea na kuonesha utayari wa kuyafanyia kazi kwa manufaa ya taifa. 


Chama hicho pia kiliahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu katika utekelezaji wa mapendekezo hayo, pamoja na kuwahamasisha Watanzania kuyaunga mkono.


Hata hivyo, Amesema CCM njia sahihi ya kufikia suluhu ya kudumu ni kupitia maridhiano ya kitaifa, sambamba na kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ghasia hizo, waliohusika, malengo yao na hatua stahiki za kuwawajibisha wahusika.


Kwa mantiki hiyo, chama hicho kimeunga mkono hatua inayofuata ya kuundwa kwa tume ya upelelezi itakayochunguza kwa kina matukio hayo, kikieleza kuwa kiko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na amani, umoja na mshikamano.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI