Na Matukio DaimaApp
Chama Cha Act Wazalendo kimesema bado kinaendelea na msimamo wake wa kutoitambua Tume ya kuchunguza matukio wakati na baada ya uchaguzi Oktoba,2025 iliyoundwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mohamed Chande Othman kwa madai kuwa tume hiyo imetoa ripoti ambayo haipo wazi.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Mei 4,2026 Makao makuu ya chama hicho Magomeni Jijini Dar es salaam,Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho Isihaka Mchinjita amesema kuwa tume imetoa ripoti ambayo haina takwimu sahihi za watu waliouawa.
Pia amesema kuwa ripoti hiyo haijataja hatua zitakazochukuliwa dhidi ya watu waliohusika na mauaji, ambapo hata idadi kamili ya watu waliouwawa hawajaiweka wazi.
Amesema kuwa, ni vyema kuwepo kwa tume huru ya umoja wa mataifa itakayotumika kufanya uchunguzi wa kina kwani Tanzania ni mwanachama wa jumuiya hiyo.
Halikadhalika Mchinjita ameongeza kuwa viongozi walioshindwa kudhibiti mauaji hayo wachukuliwe hatua ikiwemo kufukuzwa kazi kutokana na uzembe walioufanya wa kushindwa kudhibiti vurugu hizo wakati wahalifu wakipanga njama ya kufanya vurugu mita 10 kutoka kituo cha polisi kama ilivyodaiwa kwenye ripoti ya Jaji Chande.
Aidha amewataja Viongozi wanaopaswa kuwajibika ikiwa ni pamoja na wakuu wa Mikoa yote ambayo Vurugu zilifanyika na kusababisha mauaji,pamoja na Viongozi wa ulinzi na usalama walioshindwa kuzuia mauaji hayo.






0 Comments