Na Herieth Molla ,Matukio Daima Media Iringa Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Kalenga, Wilaya ya Iringa, Peter Mvula, amesema kuanzishwa kwa kituo hicho kumekuwa mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwenye jamii.
Mvula amesema kituo hicho kilianzishwa Novemba 2024 na tangu wakati huo kimekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Kata ya Kalenga kwa kutoa elimu na kuondoa hofu miongoni mwa wananchi ambao hapo awali waliogopa kuripoti matukio ya ukatili waliyokuwa wakiyashuhudia au kuyapitia.
Ameeleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa kituo hicho, Kata ya Kalenga iliyopo Wilaya ya Iringa ilikuwa ikikabiliwa na matukio mengi ya ukatili, yakiwemo ubakaji, ulawiti na migogoro ya kifamilia, hali ilisababisha pia kuongezeka kwa watoto wa mitaani.
Kwa mujibu wa Mvula, chanzo kikubwa cha matukio hayo ni unywaji wa pombe kupita kiasi, hasa katika kipindi cha mvua na msimu wa mavuno.
Aidha, Mvula amesema kituo hicho kinachofanya kazi chini ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (Tanzania Gender Networking Programme – TGNP), kimekuwa kikitumia mbinu mbalimbali kufikisha elimu ya kupinga ukatili, ambazo ni pamoja na kushiriki mikutano ya hadhara vijijini, kutembelea wananchi nyumba kwa nyumba, kutoa elimu mashuleni pamoja na kufika katika vilabu vya pombe kuzungumza na wananchi.
Ameongeza kuwa kwa sasa kituo hicho kimeongeza idadi ya wanachama kutoka 30 hadi kufikia 36, wakiwa wanatoka katika vijiji vyote vya Kata ya Kalenga.
Kwa upande wake, Marry Anthon, ambaye ni mwanachama wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kalenga, amesema kituo hicho kimeleta uelewa na ujasiri kwa wanawake na watoto, kwa sasa wanaweza kuzungumza kwa uwazi na kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili au wanapohisi viashiria vya ukatili katika maisha yao.
Aidha, Marry ameongeza kuwa elimu wanayoipata kupitia kituo hicho imesaidia kupunguza ajira za watoto pamoja na tabia ya kuwaacha watoto kwa wazee.
Alifafanua kuwa hapo awali baadhi ya mabinti walikimbilia mijini kufanya kazi za ndani na kuwaacha watoto wao vijijini, hali iliyochangia malezi duni, hata hivyo, kupitia elimu hiyo, wazazi na walezi wamehamasika kuwajibika zaidi katika malezi, huku baadhi ya wazee wakikataa kubaki na wajukuu bila mpango madhubuti wa malezi.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa, Martin Chuwa, amesema uwepo wa mashirika mbalimbali yanayoshirikiana na Serikali kutoa elimu kwa jamii umechangia kupunguza matukio ya ukatili mkoani humo, hususani katika Wilaya ya Iringa ambayo hapo awali ilikuwa ikikabiliwa na matukio mengi ya ukatili.
Chuwa ameyapongeza mashirika hayo pamoja na waratibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya, akisema mchango wao unaonekana wazi ukileta matokeo chanya kwa jamii.
Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Kata ya Kalenga kilianzishwa mwaka 2024 kupitia mpango wa Urasimishaji na Uwajibikaji wa Kijamii unaoratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).







0 Comments