Header Ads Widget

WATUMISHI WA ARDHI MKOA WA IRINGA WAKUTANA KWA KIKAO KAZI, WAPANIA KUIMARISHA UWAZI NA UWAJIBIKAJI

 

Na Matukio Daima Media, Iringa

Watumishi wa sekta ya ardhi Mkoa wa Iringa wamekutana katika kikao kazi maalumu kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka wa fedha unaomalizika na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku wakikumbushwa umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuepuka migongano ya maslahi inayoweza kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo kuhusu maadili ya utumishi wa umma yaliyofanyika sambamba na kikao hicho, Afisa Uchunguzi kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mbeya, Leonard Daudi Kansimba, alisema watumishi wa umma wanapaswa kuhakikisha maslahi ya wananchi yanawekwa mbele wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.


Kansimba alisema serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kuwawezesha wananchi kujiondoa katika umaskini kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi, lakini utekelezaji wa shughuli hizo lazima uzingatie sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.

Alieleza kuwa changamoto kubwa inayoweza kujitokeza katika utendaji wa watumishi wa umma ni pale ambapo mtumishi anapoendesha biashara binafsi inayohusiana moja kwa moja na sekta au shughuli anazosimamia kazini.

 Hali hiyo, alisema, inaweza kusababisha mgongano wa maslahi na kuathiri haki katika utoaji wa maamuzi na huduma kwa wananchi.

“Maslahi binafsi hayapaswi kushinda maslahi ya umma mtumishi wa umma anapaswa kuhakikisha maamuzi anayoyafanya yanazingatia sheria na haki kwa wananchi wote bila kuathiriwa na shughuli zake binafsi za kiuchumi,” alisema Kansimba.


Aliongeza kuwa migongano ya maslahi inaweza kusababisha upendeleo, uvujishaji wa siri za kikazi, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kupindishwa kwa sheria na taratibu kwa manufaa ya mtu mmoja au kundi fulani. Kwa mujibu wake, hali hiyo inaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa taasisi za umma na kupunguza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Kansimba aliwataka watumishi kuchagua shughuli za ziada zisizoingiliana na majukumu yao ya kikazi ili kulinda heshima ya utumishi wa umma na kuhakikisha uwajibikaji unaimarika katika taasisi za serikali.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Iringa, Rehema Kilonzi, alisema kikao hicho kimewakutanisha watumishi wa sekta ya ardhi kutoka halmashauri zote tano za Mkoa wa Iringa, Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa pamoja na watumishi wa mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya za Iringa na Kilolo.

Alisema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kubaini mafanikio na changamoto zilizojitokeza pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utendaji wa sekta hiyo katika mwaka wa fedha unaofuata.

“Kikao hiki kimetupa nafasi ya kuangalia kwa pamoja namna tulivyotekeleza malengo yetu kwa mwaka wa fedha unaoelekea kuhitimishwa na kujipanga kwa utekelezaji bora zaidi wa majukumu katika mwaka wa fedha 2026/2027,” alisema Kilonzi.

Aliongeza kuwa sekta ya ardhi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa bora, za haraka na zenye kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Mbali na kujadili utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi, washiriki wa kikao hicho walipata mafunzo mbalimbali kuhusu maadili ya viongozi wa umma pamoja na mbinu za kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa. Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa.

Naye Afisa Mipango Miji Mkoa wa Iringa, Fred Mgeni, alisema kikao hicho ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka unaoratibiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya ardhi na kuwapa nafasi ya kubadilishana uzoefu.

Mgeni alisema mikutano hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha usimamizi wa ardhi, upangaji wa miji na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwa inatoa fursa kwa wataalamu kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho la pamoja.

“Kikao hiki ni muhimu kwa sababu kinatupa nafasi ya kutathmini kazi tulizozifanya, kujifunza kutokana na mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza, pamoja na kuweka mikakati itakayosaidia kuongeza ufanisi katika mwaka wa fedha unaofuata,” alisema Mgeni.

Alibainisha kuwa pamoja na tathmini ya utekelezaji wa kazi za mwaka wa fedha 2025/2026, washiriki wamejadili masuala yanayohusu usimamizi wa ardhi, upangaji wa matumizi bora ya ardhi, utoaji wa hati za umiliki na namna ya kuboresha huduma kwa wananchi.


Mgeni aliongeza kuwa kikao hicho pia kimewapa fursa wataalamu wa ardhi kutoka halmashauri zote tano za Mkoa wa Iringa kukaa pamoja, kubadilishana uzoefu wa kikazi na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za ardhi na makazi.

Mafunzo na mijadala iliyofanyika katika kikao hicho imelenga kuimarisha maadili, uwajibikaji, nidhamu na utendaji bora wa watumishi wa umma, sambamba na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha imani ya umma kwa taasisi za serikali.

TAZAMA KUPITIA LINK HII

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI