Na Matukio Daima Media, Iringa
Maofisa Ardhi Mkoa wa Iringa wameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa kwa kuendelea kutoa elimu ya kuzuia rushwa kwa watumishi wa umma, wakisema mbinu hiyo ni muhimu zaidi katika kujenga uwajibikaji, uadilifu na utoaji bora wa huduma kwa wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa wakati wa kikao kazi cha wataalamu wa sekta ya ardhi kutoka halmashauri zote tano za Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika Ofisi za Bonde la Rufiji mjini Iringa, baada ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Victor Swella, kutoa mada kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na wajibu wa watumishi wa umma katika kulinda maslahi ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho, Afisa Ardhi, Catherine Chahe, alisema mafunzo yaliyotolewa na TAKUKURU yamewasaidia kupata uelewa mpana zaidi kuhusu masuala ya rushwa, maadili ya utumishi wa umma na wajibu wao katika kuhakikisha huduma za ardhi zinatolewa kwa haki na uwazi.
Alisema elimu hiyo imewafungua macho na kubadili mtazamo waliokuwa nao kuhusu TAKUKURU, huku akieleza kuwa taasisi hiyo imeonyesha dhamira ya kujenga ushirikiano na watumishi wa umma kwa kutoa elimu ya kinga badala ya kusubiri kuchukua hatua za kisheria baada ya makosa kufanyika.
“Mafunzo haya yametufungua zaidi na kutuonyesha namna TAKUKURU inavyofanya kazi kwa karibu na watumishi wa umma. Tumepata uelewa mkubwa kuhusu wajibu wetu na umuhimu wa kuzuia rushwa kabla haijatokea,” alisema Chahe.
Katika mafunzo hayo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Victor Swella, aliwataka wataalamu wa sekta ya ardhi kuzingatia uwazi, uwajibikaji na maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Alisema sekta ya ardhi ni miongoni mwa sekta nyeti zinazohudumia wananchi wengi, hivyo ni muhimu kwa watumishi wake kuhakikisha huduma zote zinatolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kulinda haki za wananchi.
Swella alisema TAKUKURU imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo viongozi wa serikali, watumishi wa umma, wasimamizi wa miradi ya maendeleo, madiwani pamoja na sekta mbalimbali za huduma kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu madhara ya rushwa na namna ya kuizuia.
Alifafanua kuwa mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa taasisi za umma na wananchi, kwani rushwa huathiri maendeleo ya jamii kwa kuchelewesha utoaji wa huduma, kupunguza ufanisi wa taasisi na kuondoa imani ya wananchi kwa serikali.
“Nawaomba watumishi kuhakikisha huduma zote zinazotolewa kwa wananchi zinafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa. Vita dhidi ya rushwa vinahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu ili kujenga jamii yenye haki na maendeleo,” alisema Swella.
Aliongeza kuwa TAKUKURU itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutoa elimu ya kuzuia rushwa na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuondoa mianya inayoweza kusababisha vitendo vya rushwa katika maeneo ya kazi.
Kwa upande wake, Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Iringa na Msimamizi wa Sekta ya Ardhi katika manispaa hiyo, Zera Chaula, aliishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuendelea kuratibu vikao kazi vinavyowakutanisha wataalamu wa ardhi kutoka ngazi mbalimbali kwa lengo la kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu.
Alisema vikao hivyo vinatoa fursa kwa wataalamu kujadili changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao na kupata suluhisho la pamoja litakalosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Tunaishukuru Wizara ya Ardhi kwa kuandaa kikao kazi hiki muhimu. Mbali na kujadili masuala ya kikazi, tumepata fursa ya kusikiliza mada mbalimbali kutoka kwa wataalamu waliobobea ambazo zitatusaidia kuongeza ufanisi katika kazi zetu,” alisema Chaula.
Aliongeza kuwa washiriki wamejifunza na kukumbushana masuala ya maadili ya utumishi wa umma pamoja na umuhimu wa kutanguliza maslahi ya wananchi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, alisema mafunzo hayo yamewapa uelewa kuhusu namna ya kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana nje ya ajira zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepuka migongano ya maslahi inayoweza kuathiri utendaji wao wa kazi.
Washiriki wa kikao hicho walikubaliana kuwa elimu ya maadili na mapambano dhidi ya rushwa inapaswa kuendelea kutolewa mara kwa mara kwa watumishi wa umma ili kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kujenga imani ya wananchi kwa taasisi za serikali.
Afisa Uchunguzi kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mbeya, Leonard Daudi Kansimba, alisema watumishi wa umma wanapaswa kuhakikisha maslahi ya wananchi yanawekwa mbele wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Kansimba alisema serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kuwawezesha wananchi kujiondoa katika umaskini kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi, lakini utekelezaji wa shughuli hizo lazima uzingatie sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
Alieleza kuwa changamoto kubwa inayoweza kujitokeza katika utendaji wa watumishi wa umma ni pale ambapo mtumishi anapoendesha biashara binafsi inayohusiana moja kwa moja na sekta au shughuli anazosimamia kazini.
Hali hiyo, alisema, inaweza kusababisha mgongano wa maslahi na kuathiri haki katika utoaji wa maamuzi na huduma kwa wananchi.
“Maslahi binafsi hayapaswi kushinda maslahi ya umma.
Mtumishi wa umma anapaswa kuhakikisha maamuzi anayoyafanya yanazingatia sheria na haki kwa wananchi wote bila kuathiriwa na shughuli zake binafsi za kiuchumi,” alisema Kansimba.
Aliongeza kuwa migongano ya maslahi inaweza kusababisha upendeleo, uvujishaji wa siri za kikazi, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kupindishwa kwa sheria na taratibu kwa manufaa ya mtu mmoja au kundi fulani. Kwa mujibu wake, hali hiyo inaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa taasisi za umma na kupunguza ufanisi wa utoaji wa huduma.
Kansimba aliwataka watumishi kuchagua shughuli za ziada zisizoingiliana na majukumu yao ya kikazi ili kulinda heshima ya utumishi wa umma na kuhakikisha uwajibikaji unaimarika katika taasisi za serikali.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Iringa, Rehema Kilonzi, alisema kikao hicho kimewakutanisha watumishi wa sekta ya ardhi kutoka halmashauri zote tano za Mkoa wa Iringa, Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa pamoja na watumishi wa mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya za Iringa na Kilolo.
Alisema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kubaini mafanikio na changamoto zilizojitokeza pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utendaji wa sekta hiyo katika mwaka wa fedha unaofuata.
“Kikao hiki kimetupa nafasi ya kuangalia kwa pamoja namna tulivyotekeleza malengo yetu kwa mwaka wa fedha unaoelekea kuhitimishwa na kujipanga kwa utekelezaji bora zaidi wa majukumu katika mwaka wa fedha 2026/2027,” alisema Kilonzi.
Aliongeza kuwa sekta ya ardhi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa bora, za haraka na zenye kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Mbali na kujadili utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi, washiriki wa kikao hicho walipata mafunzo mbalimbali kuhusu maadili ya viongozi wa umma pamoja na mbinu za kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.
Afisa Mipango Miji Mkoa wa Iringa, Fred Mgeni, alisema kikao hicho ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka unaoratibiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya ardhi na kuwapa nafasi ya kubadilishana uzoefu.
Mgeni alisema mikutano hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha usimamizi wa ardhi, upangaji wa miji na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwa inatoa fursa kwa wataalamu kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho la pamoja.
“Kikao hiki ni muhimu kwa sababu kinatupa nafasi ya kutathmini kazi tulizozifanya, kujifunza kutokana na mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza, pamoja na kuweka mikakati itakayosaidia kuongeza ufanisi katika mwaka wa fedha unaofuata,” alisema Mgeni.
Alibainisha kuwa pamoja na tathmini ya utekelezaji wa kazi za mwaka wa fedha 2025/2026, washiriki wamejadili masuala yanayohusu usimamizi wa ardhi, upangaji wa matumizi bora ya ardhi, utoaji wa hati za umiliki na namna ya kuboresha huduma kwa wananchi.
Mgeni aliongeza kuwa kikao hicho pia kimewapa fursa wataalamu wa ardhi kutoka halmashauri zote tano za Mkoa wa Iringa kukaa pamoja, kubadilishana uzoefu wa kikazi na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za ardhi na makazi.
Mafunzo na mijadala iliyofanyika katika kikao hicho imelenga kuimarisha maadili, uwajibikaji, nidhamu na utendaji bora wa watumishi wa umma, sambamba na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha imani ya umma kwa taasisi za serikali.











0 Comments