Header Ads Widget

MEGA COPPER YAONGEZA THAMANI YA SHABA



Yalenga uzalishaji wa cathode ya asilimia 99

📍Kilimanjaro

MKAKATI wa uongezaji thamani katika Sekta ya Madini umeanza kuzaa matunda mkoani Kilimanjaro, baada ya kampuni ya Mega Copper Co Ltd kujikita katika uongezaji wa kiwango cha ubora wa madini ya shaba kutoka asilimia moja hadi kufikia kati ya asilimia 20 na 25.

Akizungumza katika kijiji cha Kiruru, wilayani Mwanga, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ally Ng’anzo, amesema maboresho hayo yameongeza ushindani wa kampuni katika soko la kimataifa, huku China ikiwa soko kuu la sasa la mauzo ya madini hayo.

Amesema pamoja na kampuni kufikia hatua hiyo ya uongezaji thamani ili kuzalisha makinikia ya shaba, matarajio yao ni kufanya uwekezaji zaidi kwa kufunga mitambo maalum ya uongezaji thamani, ili kufikia ubora wa hadi asilimia 99. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza thamani ya bidhaa hiyo, kupanua wigo wa masoko na kuimarisha upatikanaji wa malighafi ya kutengeneza bidhaa za shaba kwa viwanda vya ndani.


Kwa mujibu wa Ng’anzo, kampuni hiyo ina wafanyakazi 65, wakiwemo 20 wa kiwandani na 45 wa migodini, hali inayochangia ajira kwa vijana wa Mwanga na maeneo ya jirani, sambamba na kukuza uchumi wa jamii inayozunguka mgodi huo.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Abel Madaha, amesema mgodi huo unaomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato, ukichangia  zaidi ya Shilingi milioni 500 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kupitia tozo ya mrabaha pekee.

Amesisitiza kuwa mgodi huo ni mfano halisi wa utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuhimiza uongezaji thamani wa madini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza mapato ya taifa, ajira na uhamishaji wa teknolojia.



Mhandisi Madaha amewahimiza wawekezaji wengine kutumia fursa zilizopo mkoani humo, akieleza kuwa Kilimanjaro ina rasilimali za madini ya metali na viwandani ambazo bado hazijaendelezwa kikamilifu.

“Ofisi ya Madini itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote ili kuhakikisha Sekta ya Madini inakua kwa kasi na kuchangia ipasavyo maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla,” amesema.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI