Utoaji wa elimu kuhusu masuala ya ukatili katika Kata ya Kalenga, Wilaya ya Iringa, umeendelea kuzaa matunda baada ya wananchi kuonesha uelewa na ujasiri mkubwa wa kufuatilia, kuibua na kuripoti matukio ya ukatili kwa mamlaka husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa ,Herieth Molla,Matukio Daima Media Iringa anaripoti
Maendeleo hayo yamebainika kufuatia tukio la hivi karibuni lililoibuliwa na mkazi wa Kijiji cha Isakalilo, kata ya Kalenga, Watson Gasper, ambaye aliripoti tukio la ukatili dhidi ya watoto watatu wa familia moja waliokuwa wakifanyiwa vitendo hivyo na baba yao mzazi.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Watson alisema alipata taarifa kutoka kwa mama wa watoto hao na kuanza kufuatilia kwa kutumia mbinu alizopata kupitia mafunzo ya Kituo cha Taarifa na Maarifa Kalenga (KC). Alieleza kuwa alihakiki taarifa hizo kwa kuzungumza na watoto shuleni pamoja na majirani ili kujiridhisha na ukweli wa tukio.
Baada ya kubaini kuwepo kwa viashiria vya ukatili, alifikisha taarifa hizo katika Kituo cha Taarifa na Maarifa Kalenga, ambacho kilishirikiana na uongozi wa kijiji pamoja na viongozi wengine wa eneo hilo kuchukua hatua stahiki. Hatua hizo zilijumuisha kuhakikisha watoto wanapatiwa hifadhi salama wakati taratibu za kisheria zikiendelea.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Kalenga (KC), Rose Wisiko, alisema tukio hilo ni miongoni mwa zaidi ya matukio 10 ya ukatili yaliyoripotiwa katika kituo hicho ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, yote yakilenga kusukuma mbele hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
Alisema mwitikio chanya wa wananchi katika kupokea elimu ya kupinga ukatili umechangia kuongezeka kwa uelewa na uwajibikaji ndani ya jamii. Kutokana na mafanikio hayo, baadhi ya wanachama wa KC wamekuwa wakiombwa kusaidia kutatua migogoro na kutoa elimu kuhusu ukatili hata katika vijiji jirani.
“Kwa sasa tunaona mabadiliko makubwa ya mtazamo. Wananchi wanaripoti matukio kwa wakati na pia wanashirikiana wao kwa wao kuelimishana kuhusu athari za ukatili,” alisema Rose.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Iringa, Martin Chuwa, alisema Serikali inatambua mchango wa kituo hicho katika kupunguza matukio ya ukatili katika Kata ya Kalenga na maeneo jirani.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa matukio ya ukatili yamepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma, hali inayochangiwa na kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa wananchi kupitia elimu inayotolewa na wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ukatili.






0 Comments