Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, William Gwajima, amewataka viongozi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kusimamia kwa karibu maadili ya taasisi hiyo na kujiepusha na watu wanaoweza kutumia nafasi zao kwa maslahi binafsi.
Gwajima ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa NaCoNGO, ambapo alisisitiza umuhimu wa uongozi wa uwajibikaji, uwazi na uadilifu katika kuendesha mashirika yasiyo ya kiserikali nchini.“Jilindeni wenyewe. Kwenye msafara wa mamba na kenge wapo lazima muwe waangalifu katika uongozi na usimamizi wa taasisi zenu,” amesema.
Waziri huyo amesema mwongozo huo mpya umeandaliwa ili kuimarisha mshikamano wa mashirika yasiyo ya kiserikali na kuyawezesha kuzungumza kwa sauti moja katika kuwasilisha maoni na mapendekezo kwa Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Gwajima, mwongozo huo unaweka misingi ya uwazi, uwajibikaji, uaminifu na kuepusha migongano ya maslahi ndani ya uongozi wa NaCoNGO huku ukisisitiza mifumo imara ya utendaji badala ya maamuzi yanayotegemea ukaribu wa watu au kujuana.
“Kujuana isiwe kigezo cha kupata fursa. Mfumo ndio ufanye kazi tunataka kumaliza ukiritimba uliopo na ikiwezekana tupewe taarifa za wale wanaozuia maendeleo ili hatua zichukuliwe,” amesema.
Aidha, amekemea vitendo vya urasimu na ukiritimba vinavyokwamisha mashirika yasiyo ya kiserikali kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, akisema baadhi ya watendaji wamekuwa kikwazo hata pale ambapo wadau wanajitolea kutumia rasilimali zao kusaidia wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakimu Maswi, amewataka viongozi wa mashirika hayo kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kufungua mifumo ya kidijitali ya mawasiliano, kuimarisha usimamizi wa taarifa na nyaraka pamoja na kujitathmini mara kwa mara ili kuongeza uwajibikaji na kuimarisha imani ya umma.
“Huu ni wakati wa mashirika kujitangaza duniani kupitia mifumo ya kidijitali, kuboresha utunzaji wa taarifa na kuhakikisha shughuli zao zinaonekana na kupimika kwa matokeo,” amesema
Mwisho










0 Comments