Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI imesema kuongezeka kwa deni la Taifa kunatokana na uwekezaji unaofanywa kupitia mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikieleza kuwa fedha hizo zinaelekezwa kwenye sekta zinazochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema ni muhimu wananchi wakaelewa kuwa mikopo ya Serikali inalenga kujenga miundombinu na huduma za kijamii badala ya matumizi yasiyo na tija.
Amesema hakuna sababu ya wananchi kuwa na wasiwasi wanaposikia deni la Taifa limeongezeka, kwa kuwa mikopo hiyo imewezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta za nishati, maji, afya, elimu, usafiri na kilimo.
Msigwa amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kuaminiwa na taasisi za fedha duniani kutokana na uwezo wake wa kukopa na kuhudumia madeni yake, hali inayoiwezesha kupata rasilimali za kuendeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi.
Aidha, amewataka watu wanaotoa taarifa kuhusu deni la Taifa kuzingatia muktadha wake badala ya kutumia takwimu zinazoweza kupotosha umma bila kueleza miradi iliyotekelezwa kwa fedha hizo.
Kwa upande wa amani, Msigwa amesema Serikali inathamini maoni na ukosoaji unaofuata sheria, lakini ikasisitiza kuwa vitendo vya fujo na uvunjifu wa amani haviwezi kuwa njia sahihi ya kuwasilisha hoja kwa kuwa vinaathiri maendeleo ya Taifa.
Pia amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kupunguza matumizi kwa kuongeza matumizi ya usafiri wa reli ya kisasa (SGR) na vyombo vingine vya usafiri wa umma katika safari za kikazi, ikiwa ni sehemu ya kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha za umma.
Akizungumzia ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi, Msigwa amesema imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika maeneo ya nishati, kilimo, utalii, usafirishaji na elimu, huku makubaliano yakijumuisha safari za moja kwa moja za ATCL kwenda Moscow, kuongezwa kwa nafasi za udhamini kwa wanafunzi wa Kitanzania na kuimarishwa kwa ushirikiano wa lugha kati ya nchi hizo mbili.TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII
Amesema Serikali itaendelea kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi na sera mbalimbali ili kuongeza uwazi, kuwajengea wananchi uelewa na kuimarisha ushiriki wao katika safari ya maendeleo ya Taifa.









0 Comments