Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao waliomaliza shule ya msingi (darasa la saba) mwaka 2025 wanalelewa katika maadili mema na kusimamiwa ipasavyo, ili kuepuka kujiingiza kwenye makundi mabaya yanayoweza kuhatarisha ndoto zao za baadaye.
Wito huo umetolewa na Mhe. Kasilda wakati akizungumza katika mahafali ya tatu ya Shule ya Msingi Askofu Josephat Lebulu iliyopo kata ya Makaya wilayani Same. Amesema ni muhimu kipindi hiki cha kusubiri matokeo ya darasa la saba kikatumika vizuri kwa kuwapatia watoto malezi na maelekezo bora.
“Tunatambua huko kwenye jamii kuna mambo mengi sana yanaweza kuwa kikwazo kwa watoto hawa ambao wamehitimu shule ya msingi. Niwaombe wazazi na walezi katika kipindi hiki ambacho watoto wanasubiri matokeo yao, hakikisheni mnawalea vyema, wapeni kazi za kufanya ili wasibweteke, pia waepusheni na makundi mabaya yanayoweza kuwaletea madhara katika kutimiza ndoto zao,” amesema Mhe. Kasilda.
Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kushirikiana kwa karibu na walimu ili kudhibiti mienendo na tabia za watoto kwa lengo la kuwajengea nidhamu na msingi mzuri wa maendeleo.
Pamoja na hayo, Mkuu wa Wilaya huyo amepongeza Taasisi za Dini, hususan Kanisa Katoliki, kwa mchango mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu. Amesema katika Wilaya ya Same, Kanisa Katoliki limewekeza shule za msingi nane (8) na sekondari kumi na moja (11), jambo linalosaidia kuinua kiwango cha elimu katika jamii.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jimbo Katoliki Same Padre Filbert Kasira, amesema wataendelea kuwekeza na kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa jamii, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wananufaika na uwepo wa taasisi hizo.
Katika risala yao, wanafunzi hao wameeleza kuwa wamefanikiwa kujifunza katika malezi bora na maadili mema na kuahidi kuwa kuwa wataendelea kusimamia malezi hayo ili waweze kufanikisha malengo yao.p
0 Comments