Na COSTANTINE MATHIAS, Itilima.
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Itilima mkoani Simiyu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Njalu Silanga amewataka wananchi kuchagua viongozi wanaotokana na CCM ili waendelee kuchapa kazi na kuwaletea Maendeleo na kuboresha upatikanaji wa huduma katika nyanja za Elimu, Afya, Maji, Umeme, Barabara, Kilimo, Mawasiliano.
Aidha Njalu amesema endapo atachaguliwa, atahakikisha anaongeza Uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi ili kuwaletea wananchi Maendeleo huku akisisitiza kuendelea kuimarisha miundombinu katika Jimbo hilo.
Akizungumza leo kwenye uzinduzi wa Kampeni uliofanyika Kijiji cha Nangale wilayani Itilima, Njalu amesema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 205/2030 imezingatia mahitaji yote ya wananchi wa Jimbo la Itilima.
Njalu amewataka Wagombea Udiwani kupitia CCM kutumia Ilani ya Uchaguzi kuomba kura huku wakieleza matarajio ya serikali ya CCM katika kutekeleza Ilani hiyo ambayo imejikita kutatua kero za Wananchi.
"Nimesimama hapa kwa kujiamini kutokana na mambo mazuri yaliyofanywa na serikali ya CCM chini ya Dkt. Samia, tumejipanga kuleta Maendeleo...kwenye Elimu wakati tunaomba kura Shule zilikuwa chache, sasa zitaendelea kujengwa kwa kiwango kizuri" amesema Njalu.
Kuhusu sekta ya kilimo, Njalu amesema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anasimamia bei ya mazao ikiwemo mbaazi na Pamba ili yaweze kuwa na soko la uhakika ambalo litamnufaisha mkulima.
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kuchagua viongozi wanaotokana na CCM ili waweze kuendelea kuboresha huduma za Barabara ili kurahisisha usafiri, usafirishaji pamoja na upimaji wa miji ikiwemo Nanga, Migati na Itilima.
Awali Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu UVCCM Taifa, MNEC Musa Mwakitinya amewataka wananchi wa Jimbo la Itilima kutobweteka bali watafute kura za Rais Dk. Samia, Mbunge (Njalu) pamoja na Madiwani wa CCM.
Amewaomba wanaCCM kumkabidhi Rais Dk. Samia miaka mitano ili aendelee kuchapa kazi kwa kuzingatia kuwa tayari ameshatekeleza miradi ya Maji pamoja na ujenzi wa Hospitali ya wilaya ambayo imeanza kutoa huduma.
"Nategemea kura nyingi za Dk. Samia Suluhu Hassan zitokee hapa wilaya ha Itilima sababu mna wapiga kura wengi kuliko sehemu nyingi Mkoa wa Simiyu, mpeni kura Rais Samia, mpeni kura Njalu Silanga, wapeni kura Madiwani wa CCM ili waendelee kuchapa kazi" amesema Mwakitinya.
Mwisho.
0 Comments