Header Ads Widget

WATALII 800 KUTOKA TUGHE WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA KILIMANJARO KUELEKEA SIKU YA UTALII DUNIANI


Watalii wa ndani 800 kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) leo Septemba 18, 2025 wametembelea Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza Utalii wa Ndani na kutambua fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta ya utalii.

Katika ziara hiyo, wageni hao walipata fursa ya kushuhudia vivutio mbalimbali vilivyomo ndani ya hifadhi, ikiwemo maporomoko ya maji, hali ya hewa ya kipekee pamoja na mimea ya aina mbalimbali inayopamba mandhari ya Mlima Kilimanjaro, maarufu duniani kama “paa la Afrika”.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu wa TUGHE Henry Mkunda alisema, “Watalii wetu wamefurahishwa na mandhari ya kipekee ya Mlima Kilimanjaro na vivutio vilivyomo ndani yake. Ziara hii imetupa uelewa mkubwa zaidi wa thamani na uzuri wa urithi huu wa dunia.”




Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Steria Ndaga, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, alisema, “Tunawapongeza viongozi na wanachama wa TUGHE kwa kuunga mkono jitihada za kutangaza utalii wa ndani. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunalinda na kutangaza vivutio hivi vya pekee. Napenda kuwasisitiza Watanzania wote kutembelea hifadhi zetu, kwani kufanya hivyo ni kuongeza pato la taifa na kuchangia ajira kwa vijana.”

Aidha, aliwahamasisha wananchi kuwekeza katika sekta ya uhifadhi kwa kusema: “Fursa za uwekezaji zipo nyingi ndani ya Hifadhi za Taifa. Tukishirikiana kwa pamoja, watanzania wanaweza kunufaika kiuchumi huku taifa likipata mapato endelevu na kuimarisha maendeleo ya kijamii.”

Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayesimamia Kitengo cha  Maendeleo ya Biashara TANAPA, Jully Bede Lyimo, aliwataka wageni hao kuendeleza utalii rafiki wa mazingira akisisitiza kuwa shughuli za utalii ni lazima tuzingatie uendelevu, faida za utalii wa ndani ni nyingi; unaongeza mapato ya serikali, unachochea ajira hasa kwa vijana, unakuza biashara ndogo ndogo, unajenga uzalendo na uelewa wa wananchi kuhusu thamani ya urithi wetu wa asili na vilevile unapunguza utegemezi wa watalii wa kigeni pekee. Hivyo, kila mmoja wetu anaposhiriki katika utalii wa ndani anachangia moja kwa moja katika maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.

Nae kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa kilimanjaro afisa uhifadhi mkuu Amri Mtekanga kwa niaba ya Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro aliwakaribisha watalii hao na kuwaelezea vivutio vilivyopo  ndani ya Hifadhi hiyo iliyobeba hivi Karibuni tuzo ya utalii duniani kama Hifadhi bora zaidi barani Afrika yenye milima na kutoa taratibu za upandaji wa Mlima Kilimanjaro.

Ziara ya TUGHE katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ni mfano halisi wa mshikamano wa watanzania katika kuunga mkono sekta ya utalii. Huku dunia ikiendelea kuhesabu siku kuelekea maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani, TANAPA inawakaribisha Watanzania wote kutembelea hifadhi za taifa ili kujivunia urithi wa asili, kuhamasika kuwekeza, na kushiriki katika kujenga mustakabali endelevu wa utalii wa nchi yetu.









Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI