Header Ads Widget

KAMISHNA KUJI AIPIGA MSASA KAMPUNI TANZU YA TANAPA (TIL)


Na. Edmund Salaho - Arusha

Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA Musa Nassoro Kuji, amewataka Watumishi wa Kampuni Tanzu ya TANAPA (TANAPA Investment Ltd - TIL) kuongeza ubunifu na kuchapa kazi kwa ufanisi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika utoaji wa huduma za ukandarasi ndani na nje ya Shirika.

Kamishna Kuji ameyasema hayo leo Septemba 18, 2025 katika kikao chake na watumishi wa kampuni hiyo tanzu ya TANAPA.

TIL ni Kampuni tanzu ya TANAPA iliyoanzishwa mnamo mwaka 2019 na lengo likiwa ni kutoa msukumo katika utekelezaji wa miradi ya Shirika pamoja na kuwa Kitega Uchumi cha Shirika katika kutekeleza miradi ya nje ya Shirika.


Kamishna Kuji ametumia fursa hiyo kuipongeza kampuni hiyo kwa kazi ambazo imeshazifanya ikiwemo ukarabati wa barabara ya Hifadhi ya Taifa Arusha, ukarabati wa kiwango cha changarawe wa baadhi ya barabara za Jijini Arusha, ukarabati wa kipande cha barabara ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kazi nyingine ambazo zimetekelezwa kwa ufanisi.

“Pokeeni pongezi kutoka kwa Bodi ya Wadhamini ya Shirika na Bodi imenituma niwaeleze kuwa inayo matarajio makubwa sana kwenu na hivyo msiwaangushe. Endeleeni kufanya kazi kwa weledi, bidii, nidhamu, kujituma, ushirikiano, upendo na mshikamano ili muweze kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa TIL” alisema Kamishna Kuji.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TIL, Mhandisi Dkt.Richard Matolo alitoa pongezi zake kwa Kamishna Kuji kwa kutenga muda wake na kuja kuzungumza na watumishi wa kampuni hiyo na kuahidi kuchapa kazi kwa ari na kasi zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na bodi ya wadhamini kupitia kampuni hiyo.

Kampuni Tanzu ya TANAPA ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kuwa miundombinu ya uhifadhi na utalii pamoja na ya kiutawala zilizopo ndani ya Hifadhi za Taifa Tanzania inakuwa katika hali nzuri wakati wote.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI