Na COSTANTINE MATHIAS, Matukio Daima-Simiyu.
BODI ya Wakurugenzi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imevitaka Vyombo vya Watumia Maji (CBWSOs), kuanza kutumia dira za Maji za malipo ya kabla, (pre paid meter) ili kudhibiti madeni yanayotokana na mauzo ya Maji.
Aidha, Bodi hiyo imevitaka vyombo hivyo kuongeza nguvu kukusanya madeni ya Maji ili kurahisisha uendeshaji huku ikiridhishwa na Utendaji kazi wa Gidui CBWSOs kwa kusimamia na kuendesha miradi ya Maji Igaganulwa, Sapiwi na Ikungulyabashahi.
Hayo yalibanishiwa jana na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Ruth Koya, kwenye ziara ya kukagua hali ya upatikanaji wa Maji katika Mkoa wa Simiyu ambapo alisema serikali ilishatoa maelekezo juu ya kuanza matumizi ya dira za malipo ya kabla.
Mhandisi Koya alisema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo ya kuondokana na Mita za kawaida ili kurahisisha utoaji wa huduma na ukusanyaji wa mapato.
"Rais Dk. Samia alishatoa maelekezo kwa Wizara ya Maji kuanza rasmi matumizi ya dira za Maji za malipo ya kabla tuondokane na kuhangaika kwenda kusoma mita ya Maji kwa wananchi... " Alisema.
Awali Meneja wa RUWASA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Emmanuel Luswetula alisema hali ya upatikanaji wa Maji katika Mkoa huo umefikia asilimia 69 kutokana na miradi mbalimbali kuendelea kutekelezwa.
Alisema katika wilaya ya Bariadi hali ya upatikanaji wa Maji umefikia asilimia 72, Busega asilimia 68, Itilima asilimia 64.9, Maswa asilimia 72 na Meatu asilimia 67.
Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, RUWASA Mkoa wa Simiyu inatekeleza miradi 27 ambayo ikikamilika itahudumia watu 168,200 sawa na ongezeko la asilimia 9.2 ya upatikanaji wa Maji ifikapo Juni 2026.
"Bajeti ijayo tumekadiria kutumia shilingi Bil. 13.5 kutoka vyanzo mbalimbali, pia programu ya visima 900 tulitengewa shilingi Bil. 1.2 kuchimba visima 35 katika majimbo Saba ya Mkoa wa Simiyu" alisema Mhandisi Luswetula.
Akiwasilisha taarifa ya Usimamizi wa Gidui CBWSOs, Katibu wa chombo hicho Mashaka Dotto Mahaja alisema hali ya upatikanaji wa Maji kwa wakazi wanaohudumiwa ni asilimia 53.4 na jumla ya wakazi 33,940 wanapata huduma ya Maji safi na salama.
Alieleza kuwa chombo hicho kinawadai wateja kiasi cha Shilingi 20,085,575 (wateja binafsi shilingi Mil. 15,504,075 na Taasisi za Serikali shilingi Mil. 4,430,500.
Mwisho.
0 Comments