Serikali kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) imefanikiwa kuanzisha vituo 206 vya kijamii vya kulelea watoto wadogo mchana na kusajili vituo binafsi 4,178 nchi nzima tangu mwaka 2021.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amesema vituo hivyo vinahudumia jumla ya watoto 11,675 huku vya binafsi vikihudumia watoto 6,154.
Aidha, jumla ya walezi 445 wamepatiwa mafunzo ya malezi na makuzi ili kuhakikisha utoaji bora wa huduma katika vituo hivyo. Mtanda alisisitiza kuwa uwekezaji katika malezi ya awali ni msingi wa kukuza rasilimali watu yenye tija kwa familia na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Bw. Sebastian Kitiku, amesema mkutano wa tathmini wa siku mbili unawaleta pamoja Maafisa Lishe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na wadau wa maendeleo ili kujadili mafanikio na changamoto za utekelezaji wa programu hiyo.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ustawi wa Jamii, Bi. Subisya Kabuje, amesisitiza kuwa washiriki wa mkutano huo wamejipanga kuibua njia bora za kuimarisha utekelezaji wa PJT-MMMAM.
0 Comments