Header Ads Widget

ALAMA YA UBORA YA AFRIKA YAZINDULIWA TANZANIA , KUFUNGUA FURSA MPYA ZA BIASHARA.

 Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam – Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Leo Julai, 31, 2026 kwa kushirikiana na Taasisi ya Viwango Afrika (ARSO), limezindua rasmi Alama ya Ubora ya Afrika, Nhini Tanzania mfumo utakaowezesha bidhaa zinazozalishwa barani Afrika kutambulika kwa alama moja ya pamoja, hatua inayotarajiwa kurahisisha biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika katika masoko mbalimbali.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, alisema ubora wa bidhaa ni nguzo muhimu katika kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinapenya na kushindana katika soko la dunia, jambo litakalochangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi shindani wenye thamani ya dola trilioni moja.

Londo alisema utekelezaji wa Alama ya Ubora wa Afrika utasaidia kupunguza muda wa ukaguzi wa bidhaa mipakani, kuongeza ufanisi wa biashara na kuimarisha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), hivyo kufungua fursa zaidi kwa wazalishaji wa Tanzania na bara zima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa Taasisi ya Viwango Afrika (ARSO), Reuben Onyangero, alisema alama hiyo itasaidia kutambulisha bidhaa zinazozalishwa ndani ya Afrika na kuongeza ushindani wake katika masoko ya kimataifa.

Alizitaka nchi za Afrika kuendelea kuimarisha mifumo yao ya ubora ili bidhaa zinazozalishwa katika bara hilo ziendelee kutambulika na kuaminika katika nchi mbalimbali, hatua itakayorahisisha biashara ya ndani ya Afrika.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, alisema Alama ya Ubora wa Afrika itazipa bidhaa za Tanzania nafasi kubwa zaidi ya kutathminiwa na kutambulika katika masoko ya Afrika, jambo litakalopanua fursa za biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Uzinduzi wa Alama ya Ubora wa Afrika ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika katika masuala ya viwango na ubora wa bidhaa, ili kuwezesha biashara kufanyika kwa urahisi zaidi na kuongeza mchango wa bidhaa za Afrika katika uchumi wa bara hilo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI