![]() |
| Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ini, Dkt. Swaleh Pazi |
Dar es Salaam:
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Mega We Care Tanzania Limited leo Julai 28, 2026 wameanza kambi ya siku mbili ya upimaji na utoaji wa chanjo bure kwa wananchi. Kambi hii inafanyika Muhimbili Sokoine Drive Medical Centre (MNHSDMC) jirani na SGR, kuadhimisha Siku ya Homa ya Ini Duniani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ini, Dkt. Swaleh Pazi amesema ugonjwa wa homa ya ini bado ni tishio kubwa.
Mwaka 2024 pekee watu milioni 1.3 walifariki duniani kote kutokana na ugonjwa huo.
"Kwa hiyo tunawahimiza wananchi wajitokeze kwa wingi kupima na kupata chanjo. Homa ya Ini B inazuilika kwa chanjo, na C ina tiba. Usiogope unyanyapaa. Vipimo hivi ni bure na vinachukua muda mfupi tu," amesema Dkt. Pazi.
Kliniki ya Homa ya Ini ya Muhimbili kwa sasa inahudumia wagonjwa zaidi ya 5,000.
Lengo la kambi hii ni kuwafikia wananchi zaidi ya 1,000 katika siku mbili.
![]() |
| Afisa Habari wa Mega We Care, Bw. Mengi Ntasimba |
Kwa upande wake, Afisa Habari wa Mega We Care, Bw. Mengi Ntasimba amesema kampuni hiyo imetoa vifaa vya uchunguzi na dawa kama sehemu ya kurejesha kwa jamii baada ya miaka 20 ya kuhudumu Tanzania.
Mmoja wa waliojitokeza, Joseph Chengula kutoka Kimara, amewapongeza waandaaji na kuwataka wananchi wengine kufika kupata huduma hiyo bure.
Kambi itaendelea hadi tarehe 29 Julai 2026.
#PimaMapema #HomaYaIni #Muhimbili #MegaWeCare











0 Comments