Morogoro | Julai 28, 2026
Serikali kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha uwezo wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kwa kuikabidhi gari jipya la utafiti litakalosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za utafiti wa misitu na ufugaji nyuki nchini.
Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser Prado Station Wagon lenye namba za usajili STN 7536 limekabidhiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Bw. Daniel Pancras, kwa kushirikiana na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), Dkt. Tuli Msuya, kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, katika hafla iliyofanyika Julai 28, 2026, Makao Makuu ya TAFORI, Morogoro.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa hafla hiyo, Bw. Pancras alisema makabidhiano ya gari hilo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ya kuendelea kuzijengea uwezo taasisi kwa kuimarisha miundombinu na vitendea kazi ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
"Nashukuru Mfuko wa Misitu Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya sekta hii kwa kuendelea kujengea uwezo taasisi. Nawasihi watumishi wa TAFORI kutunza kitendea kazi hiki ili kiendelee kusaidia taasisi kutekeleza tafiti zenye matokeo chanya kwa maendeleo ya sekta ya misitu na nyuki na kwa maslahi ya taifa," alisema Bw. Pancras.
Kadhalika, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), Dkt. Msuya, alisema kuwa kukabidhi gari hilo ni sehemu ya jitihada za Mfuko katika kuzijengea uwezo taasisi za sekta ya misitu na nyuki ili ziweze kutekeleza majukumu yake ya kitafiti kwa ufanisi zaidi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, aliishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) kwa kuendelea kuiwezesha taasisi hiyo kwa vitendea kazi vinavyorahisisha utekelezaji wa shughuli za utafiti.
"Tunashukuru Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mfuko wa Misitu Tanzania kwa kuendelea kutupunguzia changamoto za utekelezaji wa shughuli za utafiti. Gari hili litatuwezesha kuwafikia wadau kwa urahisi zaidi na kutekeleza shughuli za utafiti kwa ufanisi katika maeneo mbalimbali nchini," alisema Dkt. Mushumbusi.









0 Comments