Na Shomari Binda-Musoma
WAFANYABIASHARA wapangaji wa vibanda vinavyomilikiwa na halmashauri ya manispaa ya Musoma wasiolipia wametakiwa kuondoka.
Kauli hiyo imetolewa leo mei 21,2025 na Naibu Meya wa manispaa hiyo Naima Minga alipokuwa akihitimisha kikao cha robo ya tatu ya baraza la madiwani.
Amesema halmashauri inapaswa kukusanya mapato ya ndani ili kuweza kuwahudumia wananchi hivyo hawawezi kuwavulimia wasiolipia mapato hayo.
Naima amesema moja ya chanzo cha mapato hayo ni vibanda vya biashara vilivyopangishwa na inashangaza kuona watu wanafanya biashara na kutokulipa kwa wakati.
Naibu Meya huyo kupitia baraza hilo amemuagiza mkurugenzi wa manispaa ya Musoma kuiandaa timu yake kupitia afisa biashara kuweza kukusanya mapato." Ndugu zangu kila mmoja wetu aende kuhimiza kwenye eneo lake kila chanzo cha mapato kikusanywe ili tuweze kuwahudumia wananchi wetu.
" Kama alivyotuelekeza mkuu wa Wilaya twende tukakusanye mapato maana kwenye kipindi chote tumekuwa tukikusanya mapato kwa asilimia mia moja",amesema.
Diwani wa Kata ya Mshikamano Njofu Costantine amesema kwenye baraza hilo wamepitisha Sheria ndogo ndogo ambazo ni rafiki kuwasaidia wafanyabiashara wakiwemo wajasiliamali ili waweze kulipa.
Amesema kama alivyosisitiza mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka na Naibu Meya Naima Minga wanakwenda kuhimiza ukusanyaji mapato kwenye Kata zao.
0 Comments