Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. James Kilabuko amezindua rasmi Mwongozo wa Kitaifa kwa Watoa Huduma za Maendeleo ya Biashara ambao umelenga kukuza uchumi na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wakati pamoja na wakubwa kukuza biashara zao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, Dkt Kilabiko amesema kuwa Mwongozo huo unaweka msingi wa mabadiliko makubwa ambayo yatawawezesha wafanyabiashara kuchangia kikamilifu kwenye uchumi wa Taifa.
Amesema kuwa, ni vyema wafanyabiashara na wajasiriamali nchini Tanzania kutumia miongozo ya kibiashara inayotolewa ili kukuza na kuendeleza mitaji yao.
“Uwepo wa Mwongozo huu unalenga kuweka viwango, mwelekeo na uratibu wa huduma zinazotolewa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini, hivyo umekuja kwa wakati sahihi na tunaamini utaleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa,"amesema Dkt. Kilabuko.
Aidha amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya katika kuhakikisha mazingira ya wafanyabiashara na wawekezaji nchini yanaendelea kuwa bora.
"Kwa umuhimu wa pekee napenda kumshukuru kwa dhati, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada anazofanya katika kufungua uchumi na kuchochea biashara na uwekezaji nchini"
Ameongeza kuwa, Rais Dkt Samia ameboresha mazingira ya biashara nchini na kuchochea kuanzishwa kwa shughuli za kiuchumi nyingi katika sekta mbalimbali, shughuli hizo pia zinahitaji huduma za maendeleo ya biashara ili kuwa shindani.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wanamanchi Kiuchumi (NEEC) Beng'i Issa ameleeza kuwa Mwongozo wa Huduma za Maendeleo ya Biashara kwa Watoa Huduma za Maendeleo ya Biashara Tanzania unalenga kuboresha utoaji wa huduma za biashara ikiwa ni pamoja na ushauri, mafunzo, msaada wa kiufundi, ujuzi, uatamizi, uhusiano baina ya wafanyabiashara, mawasiliano, na usimamizi wa biashara.
"Tunategemea, Mwongozo huu unakwenda kutoa dira ya namna bora ya utoaji wa huduma za biashara Tanzania zinazoweza kuboresha biashara na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla" amesema Beng’i.
Hata hivyo, ameeleza kuwa, mwongozo huo utaleta matokeo chanya na kuwasihi watoa huduma za maendeleo ya biashara nchini kutumia Mwongozo huo kama nyenzo katika kuwahudumia wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaotekeleza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali.
Naye Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, amepongeza jitihada hizo za kuhakikisha mwongozo unazinduliwa huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kadiri inavyotakiwa na kueleza kuwa wanathamini uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yao na Tanzania.
Amesema kuwa, wataendelea kushiriki katika masuala mbalimbali ikiwemo kuunga mkono sekta ya afya, elimu, biashara na uwekezaji, kilimo, ulinzi na usalama.
Akizungumzia umuhimu wa mwongozo huo Mkurugenzi mkazi wa MEDA, Musa Lugambo amesema kuwa mwongozo huo utawasaidia sana watoa huduma kuweza kutoa huduma ambayo itawasaidia wajawasiriamali kwa ajili ya kutekeleza biashara zao.
"Tumekuwa na changamoto kwa watoa huduma ambapo unakuta kwamba huduma ambayo inayotolewa kwa wajawasiriamali inakuwa siyo ya kiwango kizuri na hivyo kushindwa kuwasaidia wajawasiriamali kuendeleza biashara zao"amesema Lugambo
Uzinduzi huo umeratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na kusimamia zoezi la uandaaji wa Mwongozo wa Kitaifa kwa Watoa Huduma za Maendeleo ya Biashara kwa udhamini wa MEDA.
Aidha umehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Serikalini, sekta binafsi, taasisi za fedha na watoa huduma wa maendeleo ya biashara na kujumuisha matukio mbalimbali ikiwemo hotuba za viongozi, majadiliano ya kitaalamu na maonesho ya huduma kutoka kwa taasisi shiriki.
0 Comments