Header Ads Widget

TUNDU LISSU NI NANI? MAMBO 7 YANAYOMTAMBULISHA MWANASIASA HUYU WA TANZANIA MWENYE MISIMAMO MIKALI

 


Katika historia ya siasa za Tanzania, ni vigumu kutaja majina ya wanasiasa walioteka hisia za watu kwa hoja, ujasiri na misimamo katika miongo miwili iliyopita bila kumtaja Tundu Antiphas Lissu.

Kwa wengi, yeye ni alama ya mapambano ya haki, demokrasia na uwajibikaji wa serikali. Kwa wengine, ni mpinzani mkorofi anayependa kugonganisha fikra na utawala. Lakini kwa wengi, Tundu Lissu ni sauti isiyotetereka katika mapambano ya haki, uwajibikaji na utawala wa sheria.

Hivi sasa, akiwa amewekwa rumande kwa tuhuma za uhaini ambazo kwa sheria za Tanzania hazina dhamana, jina la kiongozi huyu wa chama kikuu cha upinzani limerudi tena kwenye vichwa vya habari, lakini hii si mara ya kwanza.

Lissu ni mtu wa historia ndefu. Ili kumuelewa kwa undani Lissu ni muhimu kumtazama kwa jicho pana: ni nani hasa huyu mtu? Haya hapa ni mambo saba muhimu yanayomtambulisha.

Msomi aliyelelewa kwenye taaluma na tafakuri ya sheria


Tundu Lissu ni msomi wa sheria mwenye taaluma pana na ya kina, aliyezaliwa katika kijiji cha Mahambe wilayani Ikungi, Tanzania na kusoma katika Shule ya Sekondari ya Ilboru, Arusha (shule ya wanafunzi wenye vipaji maalumu kiakili) na baadaye Umbwe.

Alipata Shahada ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mnamo mwaka 1994, mojawapo ya taasisi kongwe na zenye heshima kubwa Afrika Mashariki. Hapa ndipo alipoweka msingi wa uelewa wake wa kisheria, hasa kuhusu haki za binadamu, utawala wa sheria na uwajibikaji wa taasisi za dola.

Aliongeza uzito wa taaluma yake kwa kusomea Shahada ya Uzamili (LL.M) katika Chuo Kikuu cha Warwick, Uingereza, ambapo alijikita zaidi katika sheria za kimataifa na haki za raia.

Elimu yake hii imemjenga kwenye taasisi mbalimbali za kisiasa, elimu, utafiti na utetezi wa haki.

Kwa ujumla, Lissu hajajitokeza tu kama mwanasiasa bali kama msomi anayefahamu kwa kina mfumo wa sheria na athari zake kwa jamii.

Mwanaharakati wa haki za binadamu kabla ya siasa


Lissu alianza kujitambulisha kama mwanaharakati kabla hajavaa rasmi koti la kisiasa. Tangu miaka ya 1990, alikuwa mstari wa mbele katika kutetea wananchi waliokuwa wakinyanyaswa na mfumo wa sheria usio wa haki.

Aliwahi kuwa mshauri wa kisheria wa mashirika kama vile Legal and Human Rights Centre (LHRC), Environmental Law Alliance Worldwide (ELAW), na pia alikuwa mjumbe wa Bodi ya International Federation for Human Rights (FIDH). Kazi hizi zilimuwezesha kushughulika na kesi zinazohusu mazingira, haki za binadamu, ardhi na uwajibikaji wa makampuni ya kimataifa barani Afrika.

Kama wakili alitoa msaada wa kisheria kwa watu wasio na uwezo wa kugharamia huduma hizo na alijenga jina kama mtetezi wa wanyonge.

Mfano mmoja maarufu ni kesi ya wakulima wa Loliondo, ambapo alishirikiana na wanaharakati kupinga uamuzi wa serikali kuhamisha wananchi kwa faida ya wawekezaji wa sekta ya utalii.

Lissu alitumia taaluma yake kuelezea ukiukwaji wa haki za ardhi, haki za kiraia na athari za sera za uwekezaji kwa watu wa kawaida. Mwaka 2003, aliripotiwa kuandaa nyaraka na tafiti zilizoibua athari za mikataba ya madini nchini, akieleza namna mashirika ya kigeni yanavyokwepa kodi na kuwadhulumu Watanzania kupitia mikataba isiyo na uwazi.

Umaarufu wake ulianza kupaa wakati wa utawala wa hayati Benjamin Mkapa; Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Tanzania , ambapo alijotokeza kama mtetezi mkubwa wa haki za wachimbaji wadogo wa madini na wananchi wanaoishi katika maeneo dhidi ya wachimbaji wakubwa (makampuni) yaliyopewa leseni za uchimbaji baada ya mabadiliko ya kisera yaliyofanywa na utawala wa Mkapa.

Kwa muktadha huu, haishangazai, kuona hata siasa zake zinatajwa kuendeshwa kianaharakati.

Mwanasiasa mshawishi na mwalimu wa kujenga hoja

Lissu akiwa bungeni, Dodoma

Tundu Lissu, mbali na usomi wa sheria na uanaharakati ni mwanasiasa hodari, fani iliyomtambulisha zaidi kitaifa na kimataifa. Alianza siasa akiwa na chama cha NCCR-Mageuzi, kuanzia mwaka 1992-1996, kabla ya kushawishiwa na Freeman Mbowe, kujiunga na Chadema, chama alichokitumikia kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Kupitia Chadema, Lissu ameshika nyadhifa nyingi ikiwemo Mwanasheria Mkuu wa Chama, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), na kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa taifa baada ya kumshinda kigogo aliyeongoza chama kwa zaidi ya miaka 20, Freeman Mbowe katika uchaguzi wa januari, 2025.

Mwaka 2010, kupitia Chadema, aligombea na kushinda ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki eneo lililotawaliwa na CCM kwa miongo mingi. Ushindi huu ulionekana kama ushahidi wa nguvu ya hoja na mvuto wa mabadiliko alioleta.

Hapa kwenye kuzungumza na kujenga hoja, Lissu anatajwa kuwa mwalimu mzuri, alionyesha kuanzia shuleni alipokuwa mwanafunzi na hata alipokuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Bondeni, aliyofundisha kati ya mwkaa 1995 na 1996.

'Lissu ana nguvu kubwa mbili za kuzaliwa ambazo hakuna shule inayoweza kumfundisha mtu; ujasiri na umahiri wa kuzungumza', aliwahi kuandika Mchambuzi wa siasa Tanzania, Ezekiel Kamwaga.

Akiwa bungeni, Lissu alitokea kuwa mmoja wa wabunge wenye ushawishi mkubwa. Alijijengea heshima kubwa kama mzungumzaji mahiri, mwenye uwezo wa kutoa hoja nzito zenye mashiko ya kisheria na kitaalamu. Alipewa nafasi ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambapo aliongoza mijadala mizito kuhusu bajeti, sheria kandamizi, masuala ya madini na mikataba mibovu ya serikali.

Alijulikana kwa kutumia takwimu, nyaraka na vielelezo thabiti katika kuibua hoja, jambo lililowafanya wabunge na wananchi kumheshimu hata kama hawakukubaliana naye.

King'ang'anizi mwenye matumaini na asiyekata tamaa

Mojawapo ya sifa kuu inayomtambulisha Tundu Lissu ni kuwa mtu mwenye matumaini yasiyotikisika na kutokata tamaa, hata katika mazingira ya hatari au kukataliwa mara kwa mara. Lissu amekuwa mstari wa mbele katika kudai Katiba mpya ya Tanzania kwa zaidi ya muongo mmoja, akiitazama kama msingi wa haki, uwajibikaji wa watawala, na ujenzi wa taifa lenye misingi ya demokrasia ya kweli.

Alianza kampeni hii akiwa bado Mbunge na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, akihudumu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliotoa mchango mkubwa katika Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014, akitetea kwa nguvu vipengele vya katiba pendekezwa vilivyolenga kuimarisha uhuru wa mahakama, haki za raia na mfumo wa utawala wa sheria. Wakati baadhi ya wanasiasa walijitoa au kukata tamaa kutokana na changamoto zilizokumba mchakato huo, Lissu aliendelea kusimama imara hata baada ya Bunge hilo kuvunjika bila kufikia muafaka wa kitaifa.

Katika kila jukwaa la kisiasa, iwe ndani ya nchi au akiwa uhamishoni baada ya jaribio la mauaji, Lissu ameendelea kuhubiri umuhimu wa Katiba mpya. Hata katika kampeni yake ya urais mwaka 2020, suala la Katiba mpya lilikuwa mojawapo ya nguzo kuu ya ajenda yake. Alikuwa akirudia mara kwa mara kuwa, "Katiba ya mwaka 1977 ni Katiba ya chama kimoja, haikidhi mahitaji ya taifa la vyama vingi," akisisitiza kuwa bila mabadiliko ya msingi ya kikatiba, uchaguzi wowote hauwezi kuwa huru na wa haki.

Licha ya kukataliwa mara kadhaa, kukumbwa na mateso, na hata kuhatarishiwa maisha yake, Tundu Lissu hajawahi kuacha kupigania mabadiliko hayo. Hadi leo, anapokumbwa na kesi nzito ya uhaini kutokana na msimamo wake wa "No Reform, No Election", anaendelea kusisitiza kuwa Tanzania haiwezi kusonga mbele bila katiba mpya ya wananchi. Kwa Lissu, unaweza kumuita king'ang'anizi anapolitaka jambo lake, na muhimu matumaini ni silaha ya mwisho kwakwe haamini katika kukata tamaa, bali katika kusimama imara hadi haki ipatikane.

Mpambanaji, Jasiri na mkosoaji asiyetishwa

Haijawahi kuwa rahisi kumtisha Lissu. Ana historia ya kusema kile anachokiamini bila kujali nafasi ya anayekisema. Katika kipindi chake bungeni, Lissu aliibua mijadala mikubwa kama sakata la akaunti ya Tegeta Escrow ambapo zaidi ya shilingi bilioni 300 zilichotwa kwa njia ya utata.

Aliwataja wahusika kwa majina na kuwasilisha ushahidi wa maandishi, hatua ambayo ilionyesha kiwango cha ujasiri na weledi wake. Pia aliongoza mijadala kuhusu matumizi ya fedha za umma, sheria za uchaguzi na udhaifu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akionyesha namna mfumo ulivyoegemea upande mmoja kwa faida ya chama tawala. Kwa Lissu, ukweli ama anachokiamini ni silaha yake kuu, hata kama inamgharimu maisha.

Alikosoa waziwazi serikali ya Mkapa na serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, hasa kuhusu haki za wachimbaji wadogo na rushwa katika sekta ya madini na mikataba isiyofaa kwa taifa.

Alipofika awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, Lissu hakusita kusema wazi kwamba serikali imegeuka ya kiimla, kifamilia na kikabila na ilitumia vyombo vya dola kuwakandamiza wapinzani, hali iliyowafanya baadhi ya viongozi wa upinzani kukimbilia nje ya nchi.

Katika moja ya hotuba zake kati ya mwaka 2016 na 2017, Lissu alisema "Naibu Waziri Kalemani (Medard, alikuwa Naibu wa Wizara ya Madini wakati huo), mtoto wa dada sijui wa kaka, wote Chato( Kanda ya Ziwa anakotokea Magufuli)". Hapa alikuwa akizungumzia kufukuzwa kwa aliyekuwa Waziri wa Madini, Profesa Sospeter Muhongo na kuachwa Naibu wake (Kalemani), kwa tuhuma ambazo aliamini Lissu kwamba zilipaswa kumfukuzisha pia na Kalemani, lakini alidai alilindwa kindugu.

Aliongeza kuhusu ukabila akimuhusiha Rais Magufuli ambaye alikuwa Msukuma kutoka kanda ya Ziwa na viongozi waliopewa nafasi mbalimbali serikalini; "Mkuu wa Majeshi Msukuma, (anatoka) Kanda ya Ziwa, Mkuu wa Polisi Kanda ya Ziwa, Mwanasheria Mkuu, Kanda ya Ziwa, Mwendesha Mashtaka Kanda ya Ziwa, Kaimu Jajim Mkuu, Kanda ya Ziwa, Mlipaji Mkuu wa Serikali, Kanda ya Ziwa, nani asiyejua, tupaosema nchi imeingia kwenye Udikteta ndiyo hivi".

Kumkosoa kwa kumuita Rais Magufuli 'Dikteta Uchwara", kulizua mijadala sana mwaka 2016 mpaka 2017 kabla ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana na kusurika kifo. Alitumia zaidi nafasi yake kama Mbunge na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kupata majukwaa ya kumkoa Magufuli na kuikosoa serikali kwa kina.

Mfu anayetembea na risasi mwilini


Lissu akiwa kwenye baskeli ya magurudumu matatu, Hospitali jijini Nairobi, Kenya, alipotoka kuzungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza baada ya kushambuliwa kwa risasi 16

Kama ukitaja matukio matatu maarufu Tanzania kuwahi kutokea katika miongo ya hivi karibuni, ukicha kifo cha Rais wake wa kwanza, Julius Nyerere na kifo cha Rais Magufuli, tukio la kushambuliwa kwa risasi Lissu, lilikuwa kubwa kwenye mijadala.

Septemba 7, 2017, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi 16 nje ya makazi yake mjini Dodoma baada ya kutoka bungeni. Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya kutoa madai kuwa anafuatiliwa na gari lenye namba za serikali. Hadi leo, hakuna aliyekamatwa wala kufikishwa mahakamani kwa tukio hilo. Jeshi la Polisi na Serikali mara kadhaa imesema uchunguzi wa kina unaendelea.

"Upelelezi bado unaendelea, uchunguzi hauna ukomo wa muda, kinachotoa faraja muhusika mwenyewe (Lissu) yupo nchini', alisema Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Hamad Masauni. Lakini mwenyewe Lissu anasema Jeshi la Polisi na Serikali hawajawahi kuwa na nia ya kuchunguza tukio hilo la majaribio la mauaji.

Lissu alipelekwa Kenya kwa matibabu ya haraka, kisha kuhamishiwa Ubelgiji kwa matibabu ya muda mrefu. Alifanyiwa zaidi ya upasuaji 20 kurekebisha mifupa, mishipa na viungo vilivyoharibiwa na risasi.

Alikaa kwenye matibabu kwa zaidi ya miaka mitatu, na kuvuliwa ubunge wake mwaka 2019, kabla ya kurejea nchini mwaka 2020 na kuwania Urais kupitia CHADEMA dhidi ya Magufuli, katika uchaguzi Mkuu ambao Magufuli alishinda, huku Lissu akipinga matokeo.

Kwa wengi, alinusurika kwa muujiza na tangu wakati huo, amepewa jina la utani la "mfu anayetembea." Tukio hilo lilimfanya kuwa nembo ya ukatili, na lilizua hofu ya kupungua kwa demokrasia nchini.

Mwanasiasa wa misimamo aliyepewa jina la 'Mropokaji'

Kwa tukio la kushambuliwa risasi na kunusurika kufa, kwa mtu mwingine asiye imara na misiamo, asingeweza kurejea kwenye siasa, uanaharakati ama shughuli yoyote inayoweza kuleta uadui hata mdogo. Lakini Lissu wala hajatetereka mpaka leo.

Kwa misimamo yake, amekuwa akikataa pia kushiriki mazungumzo ya maridhiano na Chama Cha Mapinduzi, CCM, akiyaita "mazungumzo hewa yasiyo na dhamira ya kweli."

Baada kurejea nchini mwaka 2020, na kugombea urais, Lissu alirejesha nguvu ya upinzani katika siasa za Tanzania, iliyoanza kudorora, baada ya mikutano ya kisiasa kufungwa. Akaendelea kukosoa mfumo wa uchaguzi Tanzania, akionyesha unaipendelea chama tawala, CCM, jambo ambalo Mamlaka na CCM wenyewe wanapinga.

Disemba 2024 Chadema chini ya mwenyekiti aliyepita, Freeman Mbowe, kilipitisha 'No Reforms, No Election', ambao ni msimamo wa kisera wa chama hicho unaotaka mabadiliko ya Tume ya Uchaguzi, sheria ya vyama vya siasa na uhuru wa mikutano ya hadhara kabla ya kushiriki uchaguzi.

Lissu amekuwa msitari wa mbele kutetea msimamo huu tangu awe mwenyekiti Januari, 2025, akisisitiza kuwa kushiriki uchaguzi bila marekebisho ni kushiriki udanganyifu. Hata pale baadhi ya wanachama wa CHADEMA walipoanza kuyumba kwenye msimamo huo, Lissu alibaki imara.

Kuanzia kwenye uchaguzi wa ndani wa chama, ambapo alipokataa kukaa pembeni na kumpisha Mbowe agombee uenyekiti, mpaka kupigia debe msimamo wa "No Reforms, No Election', Lissu alisemwa kama mropokaji.

Lakini yeye ameendelea kusimamia hilo na kuendelea kuhubiri kwa wananchi ili wamuunge mkono, msimamo ambao sasa unamgharimu sasa, amekamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa kesi ya uhaini.

Mtu wa kesi 'lukuki'


Lissu akiwa Mahakamani Dar es Salaam, April 10, 2025, baada ya kusomea mashitaka ya kesi ya pili ya Uchochezi

Aprili 09, 2025, Lissu alikamatwa akiwa mkoani Ruvuma baada ya kufanya mkutano wa hadhara kupigia debe msimamo wa "No Reforms, No Election'. April 10, 2025 akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam na akafunguliwa mashitaka ya uhaini, kosa ambalo linahusishwa na kutishia usalama wa taifa.

Kosa hili halina dhamana, na hivyo Lissu anasubiri hatma yake akiwa rumande. Hii si kesi ya kwanza, Lissu amekuwa na kesi nyingi, na nyingi zikiwa za uchochezi kwa maneno aliyoongea kwenye majukwa ya siasa, ama majukwaa mengine yanayohusisha ukosoaji wake.

"Hafungwi mtu hapa....., sikilizeni niwaambie nina kesi sita Kisutu (Mahakama), na zote za uchochezi', alisema Lissu wakati wa harakati za uchaguzi Mkuu wa 2020, akiwatoa hofu wanachama wa Chadema kwamba kesi hizo hazitamzuia kugombea Urais.

Hata hivyo, kesi ya sasa ya uhaini ni kubwa na ya aina yake. Akikutwa na hatia adhabu yake ni kifo kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Lakini kwa Lissu mwenyewe labda kwa sababu ni mbobevu wa sheria, haonyeshi usoni ukubwa wa kesi hiyo zaidi ya kuendelea na ari yake ya kisiasa.

"Msiogope hii ndiyo njia ya kwenda Ikulu kama Mandela (Nelson Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini)", anasema Lissu kuwatoa hofu wafuasi wa chama chake, waliofika Mahakamani.

Kwa wafuasi wake, wanaiona kesi hii ni kama muendelezo wa uonevu kwa wanasiasa wa upinzani. Kwa Serikali, huenda kesi hii ni jaribio la kudhibiti kile wanachokiona kama uchochezi na usalama wa taifa. Lakini kwa wachambuzi wa siasa na haki za binadamu, kesi hii ni kipimo cha hali ya uhuru wa kisiasa na demokrasia ya Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

Kesi yake inaweza kuwa mojawapo ya matukio muhimu zaidi katika historia ya kisasa ya Tanzania. Kama atapatikana na hatia, inaweza kubadilisha sura ya siasa ya upinzani nchini. Kama atashinda vita hii ya kisheria, huenda akawa alama hai ya ushindi wa haki dhidi ya woga.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI