Soko la hisa nchini Japan limefungua likiwa limeshuka kutokana na mazingira ya kusuasua yatokanayo na sera ziazobadilika kwa kasi za Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu nyongeza za ushuru.
Hapo jana Rais Trump aliliambia baraza lake la mawaziri kuwa kipindi hiki kigumu hakiepukiki lakini akasisitiza wawekezaji wamefurahishwa na maamuzi yake.
Thamani ya sarafu ya Dola imeshuka ikilinganishwa na sarafu za Ulaya na bei ya mafuta pia imeshuka kwa karibu asilimia nne.
Katika hali inayoashiria kuendelea kwa mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na China, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya China vimeanza kutoa ujumbe wa kuwahamasisha raia wake kuwa tayari kwa changamoto za kiuchumi zitakazotokana na vita vya ushuru wa kisasi vinavyoendelea kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karoline Leavitt, akizungumza na kituo cha habari cha Fox News, alisisitiza msimamo wa serikali ya Marekani wa kulinda maslahi ya kitaifa kwa kuiweka Marekani mbele kiuchumi na kuhamasisha urejeshaji wa ajira kutoka nje ya nchi.
“Sera ya Ikulu hii ni kuiweka Marekani mbele na kurejesha ajira,” alisema Leavitt.
“Hatutaruhusu tena bidhaa za bei ya chini kutoka China kuingia kwa wingi katika soko letu huku wao wakizuia bidhaa zetu kuingia kwao.”
Kwa mujibu wa msemaji huyo, Marekani haiwezi kuendelea kustawi kiuchumi ikiwa itaendelea “kuinyanyua na kuipa nguvu China” kwa kuruhusu uagizaji mkubwa wa bidhaa kutoka taifa hilo la Asia.
Leavitt aliongeza kuwa licha ya hali hiyo, kuna “sababu kubwa ya kuwa na matumaini kuhusu uchumi wa Marekani,” akibainisha kuwa kampuni nyingi zitaanza kunufaika zaidi kwa kufanya biashara ndani ya mipaka ya taifa hilo.
Katika hatua ya hivi karibuni, Ikulu ya Marekani imeweka wazi kuwa ushuru mpya kwa bidhaa kutoka China utakuwa asilimia 145 kinyume na asilimia 125 iliyotangazwa awali.
Maafisa wa Ikulu wameeleza kuwa kiwango kilichotajwa na Rais Donald Trump siku ya Jumatano ni ongezeko la asilimia 20% iliowekwa wiki chache zilizopita dhidi ya bidhaa kutoka China.
0 Comments