Header Ads Widget

MZOZO WA DRC: KWANINI JESHI LA CONGO HALIWEZI KULILINDA ENEO LA MASHARIKI?

 Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakitembea katika mitaa ya Kinshasa.

Wakati fulani jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC0, lilikuwa ni jeshi lenye nguvu, lakini sasa linahangaika kulinda eneo la Mashariki mwa nchi hiyo kutoka kwa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao wamepiga hatua kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu tangu kuibuka tena 2021.

M23 imetwaa udhibiti wa miji miwili ya kimkakati mashariki mwa DRC; Goma na Bukavu. Hivi karibuni pia walichukua udhibiti wa mji wa uchimbaji madini, Walikale, huko Kivu Kaskazini, lakini kisha walijiondoa baada ya mpango wa mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Qatar.

Mafanikio ya M23 yanashangaza. Wakati jeshi la Congo linakadiriwa kuwa na maelfu ya wanajeshi, Umoja wa Mataifa unakadiria M23 ina wapiganaji elfu tatu hadi nne, wengine kutoka Rwanda.

Mwaka 2023 DRC iliongeza matumizi ya kijeshi na kufikia dola milioni 794. Hata hivyo, kwa nini jeshi la Congo limeshindwa katika eneo la Mashariki?

Utawala wa Mobutu

Kulingana na wataalamu, jeshi la Congo liliheshimiwa sana baada ya uhuru, mapema miaka ya 1960 na 70 chini ya rais wa zamani wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Mobutu Sese Soko.

"Wakati fulani lilikuwa ni jeshi lenye nguvu, lakini baadaye lilisambaratika na kusambaratishwa," anasema Mvemba Phezo Dizolele, Mkurugenzi wa Mpango wa Afrika katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa (CSIS).

"Katika miaka ya mwisho ya utawala wa Mobutu, jeshi lilianguka vibaya. Aliunda kikosi cha Ulinzi wa Rais ambacho kilikuwa na vifaa vya kutosha - lakini hilo lilifanywa kwa gharama ya jeshi," anasema.

Mbali na ukosefu wa fedha, jeshi lilikabiliwa na changamoto nyingine baada ya makubaliano ya amani kufikiwa ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kikanda katika miaka ya 1990.

Kama sehemu ya mikataba hii, vikundi vya waasi vilipelekwa serikalini na wanamgambo wao wakaingizwa jeshini. Kufikia katikati ya miaka ya 2000, jeshi la taifa lilikuwa linaundwa na wanajeshi wa Mobutu na idadi kubwa ya waasi.

"Mchakato huu wa kuunganisha jeshi la zamani na vikundi vya waasi haukwenda sawa," anasema Richard Moncrieff, Mkurugenzi wa Mradi wa Maziwa Makuu katika shirika la Crisis Group.

"Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, kulikuwa na jeshi kitaifa, lakini kwa kweli lilikuwa ni jeshi la pande kadhaa zilizopigana hapo awali, kila moja ikiwa na ajenda yake na wakati mwingine ikiwa na ajenda zao za ndani ambazo haziendani na ajenda za serikali kuu."

Uongozi mbovu na ufisadi

Jeshi kushindwa kuwa pamoja kumesababisha kuwe na minyororo mingi ya amri sambamba na kukosekana uongozi thabiti.

"Wacongo wana uwezo wa kupigana, lakini kuna rushwa na uangalizi mdogo. Pesa zinatolewa na hakuna anayekuja na kuuliza zimetumiwaje," anasema mchambuzi wa masuala ya Afrika, Dizolele.

Dizolele anasema ufisadi huu unamaanisha ni vigumu kujua ni wanajeshi wangapi wanaohudumu katika jeshi kwa sasa, sababu mara nyingi idadi hiyo inaongezeka "kwa madhumuni ya kujinufaisha."

Moncrieff anaongeza kuwa uongozi mbovu katika jeshi unaakisi serikali kuu ya nchi hiyo, ambayo nayo iko katika mgogoro kama huo.

"Nchi ina matatizo ya kisera, matatizo ya kisiasa na matatizo makubwa ya rushwa. Jeshi ni kielelezo cha jamii na siasa wanazowakilisha," anasema.

Anasema rushwa hii ina maana kiasi kikubwa cha fedha kinachoingizwa kwa wanajeshi ni mara chache sana huwafikia wanajeshi. Wanajeshi wa eneo hilo wanalipwa malipo duni na familia zao hupata usaidizi mdogo sana.

Katika uchunguzi wa BBC mapema mwaka huu, iligundua mamluki wa Kiromania waliokodiwa kupigana nchini DRC walikuwa wakilipwa karibu dola 5000 kwa mwezi, ikilinganishwa na wanajeshi wa kawaida ambao hupokea karibu dola 100 kwa mwezi, au wakati mwingine kutolipwa.

Jeshi la Congo

Wanajeshi 14 wa Afrika Kusini walifariki hivi karibuni katika uwanja wa vita mashariki mwa DRC.

Kwa kufahamu udhaifu wa jeshi lake, serikali ya DRC imetoa wito kwa nchi za jirani kusaidia kupambana na makundi ya wanamgambo mashariki mwa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2021, kumekuwa na idadi kubwa ya maafisa wa kimataifa waliotumwa katika eneo hilo, hususan, kutoka EAC (Jumuiya ya Afrika Mashariki). Vikosi vyake vilikaa kwa mwaka mmoja Congo.

Wanajeshi wengine ni kutoka Malawi, Afrika Kusini na Tanzania walitumwa kama sehemu ya ahadi ya SADC (Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika). Na nchi jirani ya Burundi ilituma wanajeshi pia.

Lakini Dizolele anasema kujitolea kwa wanajeshi hao wa kimataifa "kunategemea uongozi wa kisiasa wa nchi hizo."

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema wanajeshi kutoka jeshi la Uganda, ambalo liko DRC kusaidia kupambana na makundi ya Islamic State, wamekuwa wakitoa msaada kwa M23.

Moncrieff anaamini Uganda inafanya hivyo ni kulinda maslahi yake katika mzozo huo.

"Uganda inaamini ni muhimu kuwa na ushawishi mkubwa katika jimbo la Ituri na inataka kuwa na ushawishi ndani ya M23 ili kuhakikisha kundi hilo halidhibitiwi na Kigali pekee," anasema.

Anaongeza kuwa mamluki na wakufunzi pia wameitwa kuisaidia nchini DRC, kwa sababu jeshi la Congo halina uwezo.

Hata hivyo, anasema wanajeshi hawa wa ziada kutoka nje hawajafanya vya kutosha kuizuia M23 kusonga mbele.

Waasi wa M23

Benki katika maeneo yanayodhibitiwa na M23 bado zimefungwa, kumaanisha kuwa hakuna pesa taslimu katika mzunguko.

Jeshi dhaifu la Congo likikabiliana na M23 walio na ujasiri, wanaoungwa mkono na Rwanda, na kundi hilo la waasi limeweza kusonga mbele.

"Inaonyesha uimara wa jeshi la Rwanda sio tu katika masuala ya mpangilio, nidhamu, muundo wa amri, mipango, mikakati na ujasusi, lakini pia katika suala la vifaa," anasema Moncrieff.

Ingawa M23 imesonga mbele kwa kasi, lakini kuendelea kushikilia maeneo hayo ni swali jingine.

Miji iliyo chini ya udhibiti wao, kama Bukavu na Goma, inakabiliwa na mzozo wa kibinadamu. Benki zimefungwa, ikimaanisha hakuna pesa taslimu katika mzunguko. Bei ya bidhaa za msingi na kiwango cha uhalifu kimeongezeka.

Kwa hali hiyo, wataalamu wanaamini ingawa M23 inaweza kuendelea kusonga mbele, lakini watapata tabu kuendelea kushikilia maeneo hayo.

"Watu wa Congo hawapendezwi na kile ambacho M23 inakifanya," anasema Dizolele.

"Raia hawaungi mkono kundi hilo. Kwa hivyo, kinachoweza kutokea ni kuibuka kwa wanamgambo zaidi."

Kwa muda mrefu, wataalamu wanasema jeshi la Congo linahitaji kufanya mageuzi haraka ili kuwa na ufanisi.

Lakini, wanasema, hili haliwezekani kwani mageuzi ni mchakato mrefu na wa gharama kubwa ambao unategemea nia ya kisiasa iliyo thabiti na imara.

"Wanasiasa wanahofia kuweka taratibu za uwazi na utendaji kazi unaoeleweka katika ofisi zao kuu. Wana hofu juu ya uwezekano wa jeshi kuwapindua," anasema Moncrieff.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI