Header Ads Widget

G-55 NA NO REFORM NO ELECTION" ZINAVYOIWEKA CHADEMA NJIAPANDA YA KISIASA




 Katika kipindi ambacho Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu, chama kikuu cha upinzani nchini humo, CHADEMA, kimejikuta kwenye mzozo mkubwa wa ndani unaoweza kubadilisha sura yake ya kisiasa kwa miaka mingi ijayo.

Mzozo wa sasa umeibuka kutokana na msimamo wa "No Reforms, No Election" unaoongozwa na uongozi wa juu wa chama, msimamo unaodai kuwa CHADEMA haitoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kama hakutafanyika mabadiliko ya kimfumo katika uchaguzi, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya katiba, sheria, na kuhakikisha kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi.

Ingawa yapo mabadiliko kadhaa yamefanyika mwaka jana kusainiwa kwa Sheria inayosimamia uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024, Sheria ya Tume Huru ya Taifa Ya Uchaguzi namba mbili ya 2024 na Sheria ya Marekebebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa namba tatu ya mwaka 2024, CHADEMA inayaona kama 'danganya toto'.

Ikapitisha azimio au msimamo wa "No Reforms, No Election" unaolenga kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka huu, mpaka kufanyike marekebisho makubwa ya mifumo na sheria za uchaguzi, kwa kile inachodai sheria na mifumo ya uchaguzi iliyopo sasa inaipendelea zaidi chama tawala.

Msimamo huo sasa unaonekana kukipitisha chama hicho kwenye mtihani mkubwa wa kuamua mustakabali wake kisiasa, hasa baada ya kibuka wanaoupinga likiwemo kundi la wanachama wanaojiita G-55 waliojitokeza hadharani, na kukoleza migawanyiko ya ndani inayotishia ushawishi wake na umoja wake.

Lilipotokea G-55 na dhana tatu juu ya 'uasi' wao



Baadhi ya wanachama wa CHADEMA wanaounda kundi la G-55 kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kupinga 'No reform No Election'.

Mwaka 1993, kuliibuka kundi la wabunge 55 waliojiita G-55 ndani ya Chama tawala chini humo, Chama cha Mapinduzi (CCM), lililotaka mabadiliko ndani ya chama ya kuleta Serikali ya Tanganyika ndani ya Tanzania. Lilitikisa sana utawala wa Rais wa wakati huo, Ally Haasan Mwinyi, na lilionekana kama kundi la waasi.

Kama si kuingilia kati kwa viongozi wakuu akiwemo Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, leo pengine kungekuwa na mpasuko zaidi ndani ya chama na kubadili siasa za nchi kwa miaka mingi. Harakati za kundi hilo, zimesalia kuwa historia kubwa Tanzania.

Miaka 32 baadae linaibuka kundi lingine G-55 ndani ya CHADEMA, linaloupinga wazi Msimamo wa No Reform, No Election.

'Wanaotaka uchaguzi ni wengi kuliko wanaotaka kuzuia uchaguzi, kwa sababu hawaoni huo muujiza wa kuzuia uchaguzi', anasema John Mrema, mmoja wa wanachama wa G-55.

No Reforms, No Election, ni msimamo wa kisera wa chama hicho uliopitishwa na Kamati Kuu katika kikao chake cha Disemba 2-3, 2024 chini ya mwenyekiti aliyepita, Freeman Mbowe kabla ya kupata baraka ya Mkutano mkuu wa Januari 21, 2025 ulioongozwa na Mbowe, mkutano ambao pia ulimchagua mwenyekiti mpya, Tundu Lissu.

Kwa kupinga namna ya utekelezaji wa msimamo huo wa chama, kundi la G-55 linaonekana kuwa kundi lingine la 'uasi' ndani ya chama, linaloasi maamuzi yaliyopitishwa na vikao halali vya vyama. Hii ni dhana inayojengwa na dhana nyingine inayohusisha makovu ya uchaguzi uliopita wa ndani wa chama, uchaguzi wa Januari, 2025. Ulikuwa uchaguzi wenye mvutano mkali kuwahi kutokea kwenye siasa za vyama vingi Tanzania. Lissu akimbwaga kigogo aliyeongoza chama kwa miaka zaidi ya 20, Mbowe katika nafasi ya Uenyekiti kwa kupata kura 513 dhidi ya 482 alizopata Mbowe.

'Uchaguzi wa ndani ndio mzizi wa yote, ukitizama asilimia kubwa ya wanaopinga No Reforms, No Election walikuwa wafuasi wa Mbowe, unategemea nini?", anasema Boniface Charles Mkazi wa Salasala. Hata hivyo dhana hii inapingwa vikali na John Mrema "sio kweli', akisema wapo miongoni mwao walikuwa wakiumuunga mkono Lissu.

Dhana ya tatu, ni kuhusishwa kwa G-55 na wapinzani wa CHADEMA walio nje ya chama, wanaotajwa kufadhili kundi hili.

"Hii ni project ina pesa nyingi, wachache wanaoiongoza kwa nyuma ni wanufaika wazuri sana pamoja na watu wao walioko upande wa pili", anaandika Godbless Lema, kwenye mtandao wake wa X na kuongeza "Nitanyoosha rula, yaliyofanyika darini yatawekwa hadharani'.

Pengine hii itasalia kuwa dhana mpaka yatakapobainika dhahiri hadharani hapo mbeleni.

Ilipo CHADEMA sasa ilipita CUF na NCCR-Mageuzi


Aliyekuwa Katibu wa CUF na mgombea Urais wa Zanzibar, Seif Sharif Maalim (kulia) akiwa pamoja na Mwenyekiti wake, Prof.Ibrahim Haroun Lipumba (katikati), aliyekuwa anawania Urais wa Tanzania na mgombea Mwenza Juma Duni katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.


Historia ya vyama vya siasa vya upinzani nchini Tanzania inatoa funzo kubwa kuhusu athari za migawanyiko ya ndani. Vyama vingi vya upinzani vimekumbwa na matatizo ya kuvunjika na kupoteza nguvu kutokana na migawanyiko ya ndani ya kisiasa, na hii inafanya kuangalia mgogoro wa CHADEMA kuwa na umuhimu mkubwa katika kuielewa hatma ya chama hicho.

Chama cha wananchi (CUF), kiliwahi kuwa chama kikuu cha Upinzani hasa Visiwani Zanzibar ilipokuwa ngome yake, ni mfano muhimu wa chama kilichopitia mgogoro wa ndani mkubwa na hatimaye kupoteza nguvu kubwa kisiasa. Mzozo kati ya Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba na aliyekua Katibu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, ukaua nguvu kubwa ya CUF bara na Visiwani. Japo Chama hicho kinaendelea kupumua, lakini uhai wake leo, hauwezi kufika hata robo ya uhai wa CUF ya miaka ya 1990 na 2000.

Hadithi inafanana na chama NCCR Mageuzi, kilichokuwa chama kikuu cha upinzani kwa upande wa bara katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi wakati huo na Waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Augustine Mrema, alishika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa Rais dhidi ya Benjamin Mkapa wa CCM, kwa kupata 27.7% ya kura. Ndiye aliyemfanya baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kupanda jukwaani kumpigia 'debe' Mkapa. Lakini migogoro ya ndani ya chama, ikakiporomosha chama hicho mpaka leo.

Kwa CHADEMA, mgogoro wa sasa na ilichokipita katika uchaguzi wao wa ndani wa Januari, unaonyesha wazi kuwa hauko mbali na mifano ya karibu ya vyama vya upinzani nchini Tanzania vilivyokuwa na nguvu zaidi yake lakini vilipoteza nguvu hiyo na umaarufu kutokana na migawanyiko ya ndani.

Hii inaonyesha wazi kwamba kama kitaendelea kuikumbatia migogoro hii ya ndani kinaweza kupita na kuishia kule kule ilikopita CUF na NCCR-Mageuzi: kupoteza umaarufu wake na nafasi yake katika ushindani dhidi ya chama tawala.

Kutoka waraka wa mabadiliko, wabunge wa 'Covid-19' mpaka G-55, CHADEMA kuvuka?



Halima Mdee (kulia), Ester Matiko (Kushoto) na Ester Bulaya (katikati), ni miongoni mwa wabunge 19 wanawake wenye mzozo na CHADEMA mpaka leo

Mivurugano ndani ya CHADEMA ni ya kihistoria. Ilianza muda mrefu, tofauti yake ni ukubwa, wahusika na mazingira ya mizozo husika. Ukiacha ya Chacha Wangwe, Mwaka 2013 -2015 aliyekuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho, bwana Zito Kabwe, pamoja na mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA, Dk.Kitila Mkumbo na mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba walivuliwa uongozi kwenye chama na baadaye kufukuzwa kwa kile kilichoelezwa kutaka 'kumpindua' Mbowe.

Waraka wa mwaka 2013, uliotaja wahusika wake kwa majina ya M1, M2 na M3, ulieleza kutaka mabadiliko makubwa ndani ya chama ukimuelezea Zitto kama kinara atakayesimamia mabadiliko hayo kuchukua nafasi ya Mbowe. Japo Zitto alisema waraka ulimuhusu yeye lakini hakuwa ameuona mpaka alipoitwa kwenye Kamati Kuu, CHADEMA ilivuka kwa kiasi chake mgogoro huu.

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 2015, CHADEMA ikaanza kuwa na migogoro ya ndani na wabunge wa chama hicho walioanza kuunga mkono juhudi kwa kuamia CCM. Hapo hapo ikawa na kitendawili cha ama iwasilishe majina ya wabunge wa viti maalum ama la ili waweze kuteuliwa kuingia bungeni, kwa kuwa hawakukubaliana na matokeo ya urais.

Mzozo ukaibuka baada ya kundi la wabunge 19 wanawake wakiongozwa na Halima Mdee, walipachikwa jina la utani la 'Covid-19' kutoka Chadema kufanya uamuzi wenye utata wa kwenda bungeni na kuapishwa na kuwa wabunge wa Bunge la 12.

Mpaka leo bunge linakwenda kuvunjwa chini ya miezi mitatu ijayo, mzozo huo hauna hatma. CHADEMA iliwafukuza, lakini wabunge hao wameendelea kuwepo mpaka leo.

Mgogoro ulioliingiza mpaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, maswali yakiwa mengi. Wameteuliwaje? na nani? na nani kapeleka majina bungeni wakati CHADEMA imekataa kutoa ridhaa?Chama kikaja kuwafukuza, lakini wapo bungeni, kwanini? ikiwa sheria inasema Mbunge lazima atokane na chama, na akifukuzwa uanachama na ubunge wake unakoma?

Kwa muktadha wa mgogoro wa sasa, na ukaribu wa muda wa Uchaguzi Mkuu, mazingira yanaiweka njia panda CHADEMA.

Uamuzi ni mmoja tu ama 'kusuka au kunyoa



CHADEMA sasa iko kwenye njia panda. Kila upande (wanaounga na wasiounga mkono No reform, No Election) una hoja yenye nguvu, lakini pia kila uamuzi unakuja na gharama zake. Kusimamia msimamo wa "No Reforms, No Election" kunaweza kuipa taswira ya chama cha msimamo thabiti, lakini pia kunaweza kuwaweka wanachama wengi nje ya mfumo wa siasa kwa miaka mingine mitano.

Kwa upande mwingine, kuwaruhusu wanachama kushiriki uchaguzi huku msimamo wa kitaifa wa chama ukiendelea unaweza kuonyesha ustahimilivu na ufanisi wa kisiasa, lakini pia kuna hatari ya kupokea lawama za kutokuwa waaminifu kwa misingi ya harakati.

Lakini vyovyote itakavyokuwa lazima CHADEMA iamua kusuka ama kunyoa. Ama wote waendelee na msimamo ama wote wauache msimamo wa No reform, No Election.

Ikiamua kuendelea na msimamo Je CHADEMA itaweza kuikabili dola kuzuia Uchaguzi? ni jambo rahisi? kwa gharama ipi na ya nani? pengine inazo mbinu, ni jambo la kusubiri. Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Stephen Wasira, na Emmanuel Nchimbi, katibu Mkuu wa CCM na Mgombea mwenza (Makamu wa Rais) kwa Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2025, kwamba uchaguzi upo na hakuna mamlaka yenye uwezo wa kuzuia uchaguzi usifanyike.

Wapo wanaojaribu kuwatoa kwenye njia panda waliyo nayo CHADEMA. Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa yeye anashauri chama hicho kuketi meza moja na G55′ ili kumaliza mzozo.

"Rafiki zangu Lissu , Heche (John ) Lema (Godbless) na Mnyika (John) tafuteni namna mkae na G55 yenu. Tupo tayari kusaidia majadiliano haya kati ya uongozi wa chama na G55 ili tuendeleze utamaduni wa mazungumzo pale tunapotofautiana kimitazamo," amesema.

Lakini kama Ilishindikana kukaa pande mbili wakati huo wa mizozo ya kina Zitto Kabwe na Mkumbo, haionekani kuwezekana kwa kina Halima Mdee na wabunge wenzake 19, itawezekana kwa kina John Mrema leo na G-55? Maswali haya ndiyo yanazidi kuongeza mjadala wa hoja ya mustakabali wa chama hicho.

Kwa sasa, uongozi wa CHADEMA unapaswa kutumia busara ya hali ya juu. Kupuuza hoja za G-55 kunaweza kuwa kosa la kisiasa, lakini kuzisikiliza kunaweza kuwafanya waonekane dhaifu, kosa lingine. Vyovyote itakavyokuwa, kujenga mshikamano na kuepuka kile kilichowapata vyama kama CUF na NCCR-Mageuzi ndiyo njia pekee ya kukiepusha kupoteza nguvu na ushawishi wake.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI