Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yusuf Masauni ameelekeza Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA)Morogoro kusaidia taifa kutokana na miradi inayowekezwa nchini kupitia Biashara ya Kaboni.
Wazuri Masauni aliyasema hayo mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya Mafunzo kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Biashara ya Kaboni na Shughuli za Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC).
Alisema NCMC itumie wataalamu wake kadili inavyoweza kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujikita zaidi kwenye biashara hiyo.
Alisema wananchi wanapokuwa na elimu ya kutosha katika Biashara ya Kaboni ambayo sasa imekuwa ikiangaliwa zaidi kwa kuongeza maendeleo ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa ujumla itasaidia katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
“Ni imani yangu kupitia kituo hiki tutaifaidisha taifa katika maeneo mawili, kwanza kwenye fursa ambazo zinaweza kutupatia fedha taifa pamoja na kusaidia kuratibu miradi itakayopunguza gesi joto katika dunia,”alisema Waziri Masauni
Waziri Masauni alisema mataifa ya nje yamekuwa yakija nchini kuwekeza kupitia Biashara ya Kaboni lakini wananchi wachache ndio wenye taarifa na wengi wao hawana uelewa woqote.
Pia alieleza kuwa uratibu wa Biashara ya Kaboni chanzo chake kikubwa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha na hewa ya kaboni kutokana na shughuli mbalimbali za uchumi na athari za mabadiliko ya tabianchi hata kama Afrika mchango wake sio mkubwa lakini athari zake zinaikimba nchi.
Aliongeza kwa Sasa imeshuhudia vyanzo vya maji vikikauka na sekta nyingi zikiathirika kama vile kilimo, maji, nishati pamoja na fukwe kuathirika ambapo maji huingia katika makazi ya watu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Shaka Hamdu Shaka akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Adam Malima, alisema kama mkoa tayari vipaumbele vimewekwa ili kuona wananchi wananufaika na biashara hiyo kwa kutunza misitu.
Aidha wamezijengea uwezo mamlaka ya serikali za mitaa kwa maana vijini na vitongoji ili waweze kuingia kwenye biashara hiyo ya Kaboni.
Shaka alisema wamekuwa wakipeleka makundi mbalimbali ya viongozi kwenda Kijiji cha Tanganyika kujifunza namna wanavyonufaika na biashara ya kaboni, hivyo watatumia uwepo karibu wa kituo hicho ndani ya mkoa kunufaika zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu alisema suala la uelewa juu ya biashara ya kaboni kwa wananchi bado ni mdogo hivyo wamekuwa na jukumu la kuongeza uelewa katika ngazi mbalimbali juu ya biashara ya kaboni ili wengi waweze kuifanya.
Mwisho.







0 Comments