Na Matukio Daima Media
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, CPA Nyakaho Mturi Mahemba, ameipongeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa mafanikio ya kusajili waandishi wa habari 4,519 na kuwapatia ithibati 3,655 hadi kufikia tarehe 7 Julai, 2026.
CPA Nyakaho ametoa pongezi hizo leo, Julai 7, 2026, alipotembelea banda la JAB katika Kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alipata maelezo kutoka kwa Afisa wa Bodi Bi. Editha Mayemba kuhusu majukumu ya Bodi ya kusimamia ithibati, kuimarisha maadili na weledi wa taaluma ya habari pamoja na mipango ya kuanza kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari.
Amesema hatua inayofuata kwa JAB inapaswa kuwa ni kuanza kutekeleza mpango wa mafunzo ya kitaaluma kwa waandishi wa habari, akieleza kuwa si lazima mafunzo hayo yaanze na idadi kubwa ya washiriki, bali jambo la msingi ni kuanza utekelezaji wake ili kuendelea kujenga uwezo wa waandishi na kuimarisha taaluma ya habari nchini.Katika ziara hiyo, wageni wengine waofika banda la JAB ni Mtakwimu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Chacha Nyamuhanga na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Abbas Kayanda, ambaye alisisitiza umuhimu wa maafisa habari wa wizara na taasisi za umma kujisajili na kupata ithibati kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari.














0 Comments