Na Mwandishi wetu, Matukio Daima App, Itilima.
MWALIMU Bahati Suguti, amehukumiwa kwenda jela kifungo cha miaka mitatu katika Mahakama ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu katika kesi ya wizi wa mitihani iliyokuwa inamkabili yeye pamoja na walimu wenzake watano ambao wameachiwa huru.
Katika Kesi hiyo jinai namba 27062/2024 iliyokuwa inaendeshwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Robert Kaanwa, ambapo walimu hao sita walikabiliwa na makosa mawili ambayo ni kula njama na kutenda kosa pamoja na kusaidia wanafunzi kutenda kosa la udanganyifu.
Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Jaston Haule alielezea mahakama hiyo kuwa, walimu hao katika nyakati tofauti walitenda makosa hayo kinyume cha sheria.
Alisema kuwa kosa la kwanza walimu hao ambao ni Bahati Suguti, Stephano Daud, Fauzia David, Mwita Boniface, Masatu Jepharine na Salome Aron walikula njama ya kutenda kosa la kusaidia wanafunzi wa darasa la nne kutenda kosa la udanganyifu katika vyumba vya mtihani.
Mwendesha mashtaka huyo alieleza kuwa Mnamo tarehe 25/10/2023 na tarehe 26/10/2023 katika shule ya msingi sunzula B ndani ya wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu walimu hao walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika kosa la Pili alidaiwa kuwa mnamo tarehe 25 na 26 mwezi Oktoba, 2023 katika shule ya msingi Sunzula B ndani ya wilaya hiyo kwenye mitihani ya upimaji ya darasa la nne ikiwa inaendelea, washtakiwa hao waliwasaidia wanafunzi wa darasa la nne kutenda kosa la udanganyifu katika vyumba vya mitihani.
Haule alibainisha kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume na kinyume na kifungu cha 23 na 24 vya sheria ya baraza la taifa la mitihani sura ya 107 Kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2019 viki somwa pamoja na kanuni ya 16(11)(c) ya kanuni za mitihani ya mwaka 2016 kama ilivyo tangazwa kwenye gazeti la serikali namba 89 la mwaka 2016.
Jumla ya mashahidi tisa na vielelezo 04 vilitolewa na upande wa mashtaka, katika kesi hiyo ambapo Mahakama iliwakuta na kesi ya kijibu ndipo walitakiwa kujitetea kujibu tuhuma zinazowakabili.
Baada ya kujitetea washtakiwa wote, Mahakama ikamtia hatiani mshtakiwa namba moja, Mwalimu Bahati Suguti na Hakimu Kaanwa akamhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini Milioni tano.
Washtakiwa wengine watano katika kesi hiyo ambao nao walikuwa walimu, Hakimu Kaanwa aliwaachia huru baada ya kuwakuta hawana hatia, ambapo mwalimu aliyekutwa na hatia alipelekwa gerezani baada ya kushindwa kulipa faini.
MWISHO.
0 Comments