Na Josea Sinkala, Mbeya.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema kwa kipindi cha mwezi Juni, 2026 limefanikiwa katika matukio mbalimbali kutokana na mikakati iliyojiwekea na kufanikiwa kuwatia nguvuni jumla ya watuhumiwa 239 wa uhalifu ikiwemo Mauaji, kujeruhi, kubaka, kupatikana na silaha bila kibali na matukio ya wizi.
Akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amesema miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa na upelelezi wa kesi zao kukamilishwa tayari walishafikishwa mahakamani.
Aidha, watuhumiwa watatu ambao ni Yella Mboya [27] mkazi wa Tunduma Mkoani Songwe, Furaha Mboya [25] mkazi wa Isongole na Elisa Mboma [43] mkazi wa Isongole wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya Bibi yao aitwaye Mary Mwasile [70] aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Isongole.
Kamanda Kuzaga amesema tukio hilo lilitokea Juni 28, 2026 saa nne asubuhi huko katika Kijiji cha Isongole, Kata ya Santilya, Tarafa ya Isangati wilayani Mbeya ambapo Mary Mwasile alikutwa ameuawa ndani ya nyumba yake kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni.
Amesema kufuatia tukio hilo, Polisi Mbeya kupitia Kikosi maalum cha Askari wa kuzuia na kupambana na matukio ya mauaji ilianza ufuatiliaji wa tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu na uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio ni imani za kishirikina.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari Wanyamapori [TAWA] linawashikilia watuhumiwa watatu, Shughuli Halezya [50], Shabani Matulu [36] na Baraka Mwaluswaswa [26] wote wakazi wa Lualaje kwa tuhuma za kupatikana na Silaha aina ya Gobole bila kibali ambapo walikamatwa Juni 30, 2026 katika msako uliofanyika huko katika Kijiji cha Bitimanyanga, Kata ya Mafyeko Wilayani Chunya.






0 Comments