Na Fadhili Abdallah,Kigoma
POLISI mkoani Kigoma imesema kuwa uchunguzi wa awali wa mwili wa Suez Dani Maradufu dereva wa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA John Heche umefanyika na sampuli za vitu mbalimbali kwenye mwili wa dereva huyo zimechukuliwa kwa kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa ofisini kwake kuhusu uchunguzi huo alisema kuwa kwa sasa wanasubiri kufanyika kwa uchunguzi huo wa kisayansi ndipo waweze kutoa taarifa ya uchunguzi ya nini kimetokea kwenye kifo hicho.
Kamanda Makungu alisema kuwa uchunguzi huo umehusisha madaktari bingwa kutoka hospitali ya Rufaa ya Bugando, hospitali ya mkoa Geita, Hospitali ya mkoa Dodoma, Afisa Mwandamizi kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali, viongozi wa CHADEMA na timu ya uchunguzi kutoka ofisi ya Mkuu wa upelelezi polisi mkoa Kigoma.
Wakati polisi wakitoa taarifa hiyo ya awali ya uchunguzi, Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kinataka uchunguzi wa kina kufanyika na kutoa majibu sahihi kwani uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kuna sintofahamu ya kifo hicho wakituhumu kuwa kifo hicho siyo cha kawaida.
Naibu Katibu Mkuu CHADEMA, Aman Golugwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo wa awali kwenye hospitali ya mkoa Kigoma Maweni alisema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha hakuna jeraha la ndani au la nje kuhusu sababu ya kifo hicho Zaidi ya kuonekana mshipa mkubwa unaopeleka damu kichwani kuonekana umepasuka ikionyesha ni shinikizo kubwa la damu lililosababisha kifo hicho.
Golugwa alisema kuwa sampuli mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo baadhi ya nyama za mwili, maini, figo, machozi, kucha, nywele na damu kuonyesha kwamba ni kitu gani kimesababisha kifo hicho kama sumu au kitu kingine lakini akieeleza kuwa wana mshaka kwamba kifo hicho siyo cha kawaida.
Baada ya uchunguzi huo wa awali ibada ya mwili wa marehemu ilifanyika katika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni na safari ya kuelekea Tarime mkoani Mara kwa mazishi ilianza ikitarajiwa marehemu kuzikwa Jumapili ya Julai tano mwaka huu.









0 Comments