NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Alois Ndakidemi ameshiriki kama mgeni rasmi na kuongoza harambee ya ujenzi wa Kanisa katika Usharika wa Kiwalaa, Dayosisi ya Kaskazini, katika jimbo la Moshi vijijini.
Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada iliyo ongozwa na Askofu mstaafu wa KKKT na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Onaeli Shoo.
Wengine walioshiriki ilikuwa ni pamoja na Msaidizi wa Askofu Mchungaji Msanya, Mkuu wa Jimbo Mchungaji Mrema, Mchungaji Mmanga wa Usharika wa Kiwalaa, Wachungaji wastaafu na wale waliotoka Sharika mbalimbali, Diwani wa Kata ya Mbokomu Raphael Materu, viongozi mbalimbali wa Serikali, wageni mbalimbali wakiwepo Washarika wa Kiwalaa waliopo nje ya Mbokomu na wale wanaoishi Mbokomu, na Kwaya kutoka Dar es Salaam.
Akiongea katika ibada hiyo, Baba Askofu alitumia nafasi hiyo kuhimiza jamii kuendelea kuchangia ujenzi wa makanisa, ili watu wapate nyumba za ibada, jambo ambalo pia litasadia kupunguza matendo maovu yaliyokithiri katika jamii.
Akisoma risala mbele ya Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Kanisa hilo alisema kuwa katika ujenzi huo hadi sasa tayari wameshatumia kiasi cha Shilingi Milioni
184,269,781 na hadi kukamilika zitahitajika jumla ya Shilingi Milioni 700 ambapo kanisa hilo jipya linalojengwa litakuwa na uwezo wa kuingiza Wakristo 800 kusali pamoja.
Akiongea katika harambee hiyo, Mbunge Ndakidemi alimshukuru sana Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Shoo kwa kuridhia ushiriki wake katika shughuli hiyo muhimu ya Kanisa.
Aliusifu uongozi wa Kanisa hilo kwa ushirikiano mkubwa uliopo na Serikali katika miradi mbalimbali inayosaidia wananchi katika maeneo ya Afya, Elimu na Elimu za Kiroho na kuwaomba wadau wote katika ujenzi wa Kanisa hilo washiriki kikamilifu kutoa michango yao ili hiyo kazi ya kumtukuza Mungu ikamilike kwa heshima.
Akitoa taarifa baada ya harambee hiyo, Ndakidemi alisema jumla ya Shilingi Milioni Mia Moja na Sita Laki Saba na Elfu Mbili zimeweza kuchangishwa zikiwa ni pesa Taslimu na Ahadi.
Katika harambee hiyo Mbunge alichangia kiasi cha Shilingi Milioni Tano taslimu kama mchango wake na kuwashukuru sana watu wote walioshiriki kwa majitoleo yao ya kuijenga Nyumba ya Mungu.
Akitoa neno la shukrani baada ya harambee, Baba Askofu Dkt. Fredrick Onaeli Shoo aliwashukuru sana watu wote walioshiriki katika harambee hiyo iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa namna ya pekee alimshukuru Mbunge Ndakidemi kwa ushiriki wake kama mgeni rasmi na kwa mchango wake kwa kanisa.
Mwisho.
0 Comments