Na Shomari Binda-Musoma
KADA wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) na mstafu wa heshima wa Jeshi la Wananchi Tanzania( JWTZ) Jumanne Munema ametangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Musoma mjini.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Matukio Daima amesema moja ya sababu iliyompa msukumo wa kugombea ni kuinua uchumi wa wananchi na wakazi wa jimbo la Musoma mjini
Amesema yeye kwa kuwa ni mzaliwa.wa Kata ya Nyasho Manispaa ya Musoma yapo mabadiliko ya kimaendeleo ndani ya Musoma kwa leo tofauti na miaka aliyozaliwa ambayo hayapaswi kubezwa.
Munema amesema yeye amekuja kuendeleza kasi ya maendeleo kwa miradi mipya na kuendeleza iliyopo kwa kushirikiana na wananchi na waadau mbalimbali wa maendeleo anayefahamiana nao.
Amesema vipo vipaumbele 7 anavyokuja navyo ambavyo akivisimamia iwapo wana CCM wakimpa ridhaa ya kupeperusha bendera kutakuwa na mabadiliko makubwa ya wananchi ikiwemo kiuchumi jimboni humo.
Mtia nia huyo anayedai kulitumikia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa utiifu mkubwa na kustafu kwa heshima amekusudia kutafuta wawekeza wakubwa katika kipaumbele cha kwanza ili kuinua uchumi wa wananchi wa Musoma.
Amesema mkoa wa Mara ni moja ya mikoa inayoongoza kwa kuwa na ng'ombe wengi hivyo akipatikana mwekezaji wa kiwanda cha maziwa vijana wa jimbo la Musoma mjini watapata ajira na kujiinua kiuchumi.
Licha ya uchumi kuinuka kupitia uwekezaji wa kiwanda cha maziwa zipo rasilimali nyingine nyingi zikiwemo za madini,uvuvi na uwezeshaji wananchi kiuchumi ambazo zikitumika amedai kumfanya kila mwananchi kumudu kuendesha maisha.
" Yapo mambo ambayo yamefanyika kwenye mji wetu wa Musoma ambayo yanapaswa kupongezwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya 6 chini ya Mama shupavu Dkt.Samia Suluhu Hassan na mbunge anayemaliza muda wake mheshimiwa Vedastus Mathayo.
" Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni mbunge amefanya kazi nzuri lakini kwa kuwa Chama cha Mapinduzi ( CCM) kinayo hazina ya wanachama wanaoweza kushika uongozi nimekuja kumsaidia ili kusukuma kasi ya maendeleo",alisema.
Amesema licha ya mkazo kwenye suala la uchumi vipo vipaumbele vingine vya kutilia nguvu vikiwemo vya elimu,afya,mazingira,miundombinu,maji na ujasiliamali shirikishi.
Munema amesema hivyo ni vipaumbele 7 ambavyo ataanza navyo iwapo atapewa imani na kuaminiwa kuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Musoma mjini.
Aidha Munema ameipongeza serikali ya awamu ya 6 chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea wananchi maendeleo kwa kasi katika sekta mbalimbali.
Amesema miradi mingi ya kimkakati imetekelezwa ndani ya kipindi kifupi na anastahili kulipwa kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kwenye uchaguzi wa mwaka huu ifikapo mwezi oktoba.
0 Comments