Handeni, Tanga
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetoa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za kushughulikia malalamiko kupitia mradi wa RISE kutoka ngazi ya vijiji, kata na wilaya katika halmashauri ya wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Akifungua mafunzo hayo, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Handeni ambaye pia ni Afisa Utumishi, Bi. Gladness Mwano amezitaka kamati za malalamiko kupokea na kutafutia utatuzi malalamiko ya wananchi katika maeneo yatakayoathirika na mradi wa ujenzi wa barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami wilayani humo.
"Mradi utakapoanza kutekelezwa katika maeneo yetu, kutakuwa na changamoto zitakazojitokeza, sisi kama kamati ambao tunawawakilisha wananchi wengi kwenye maeneo yetu tunatakiwa tuzingatie mafunzo ili tuweze kupokea na kuhakikisha tunayafanyia kazi malalamiko na kuwatendea haki wananchi kwa niaba yao", amesema.
Ameongeza kuwa barabara zikitengenezwa wananchi watasafirisha mazao yao sokoni kama mahindi na machungwa, wawekezaji wataongezeka na soko litakuwa na kupelekea kuongezeka kwa uchumi wa mwananchi mmoja halmashauri na hata taifa kwa ujumla.
Naye, Meneja wa TARURA wilaya ya Handeni, Mhandisi Judica Makyao amesema kuwa mradi wa RISE ni wa ushirikishwaji wa wananchi lakini pia kufungua fursa za kiuchumi na mradi unatekeleza ujenzi wa barabara ya Sindeni-Kwedikwazu (Km 38) na Michungwani - Bondo - Kwadoya (Km 19) zote zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Naye, Mkufunzi wa mafunzo hayo, Bi. Beatrice Mchome amesema kuwa serikali inalengo la kuleta mradi ambao wananchi watanufaika na kufurahia ili kuhakikisha hayo taarifa mbalimbali za utekelezaji wa mradi zimeandaliwa na elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi ili kupunguza malalamiko.
Wakizungumza kwenye mafunzo hayo baadhi ya wanakamati wameipongeza serikali kwa mafunzo hayo ambapo wameahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kujitolea ili kuwasaidia wananchi wenzao.
0 Comments