Na Ashton Balaigwa,MOROGORO
MTANDAO wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji(MVIWAMORO) umeanzisha kampeni inayowalenga vijana kushiriki katika upandaji wa miti ya aina mbalimbali zaidi ya 5000 katika wilaya ya Mvomero na Kilosa Mkoani Morogoro ili kukabilina na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.
Kampeni hiyo inayofahamika kama Youth Green tayari vijana hao wameshapanda jumla ya miti 1800 katika wilaya hizo za Mvomero na Kilosa ukishirikisha makundi mbalimbali ya vijana.
Akizungumza katika zoezi la upandaji wa miti katika wilaya ya Mvomero,Mratibu wa MVIWAMORO,Joseph Sengasenga,alisema kwa kuanzia tayari wameshapanda jumla ya miti 1980 katika vyanzo vya maji na pembezoni mwa kingo za mito mbalimbali ili kudhibiti mmomonyokowa udongo na uharibifu wa Mazingira ambao umekuwa tishio katika wilaya hizo na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
Sengasenga alisema mpango huo wa miaka miwili tayari umeshashirikisha jumla ya vijana 214 wameanza kupanda miti hiyo ni kuunga mkono mkakati wa Serikali katika kutunza vyanzo vya maji na kudhibiti uharibifu wa mazingira ili kuepukana na majanga mbalimbali ikiwemo mafuriko.
Naye Abdalah Sultani kutoka MVIWAMORO,akiongea na kundi hilo la vijana alisema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiathiri maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro hivyo ili jambo hilo sio la kuiachia Serikali pekee bali na jamii inapaswa kutoa mchango wake ikiwemo kundi hilo la vijana.
Alisema athari za mabadiliko ya tabianchi sio tu zimekuwa zikiathiri mazingira lakini zimekuwa zikisababisha pia kutokea mafuriko yasiyotarajiwa na kusababisha kuharibika kwa miundombinu mbalimbali kama madaraja na barabara hivyo ni muhimu kupandwa kwa miti .
Mwenyekiti wa Kijiji cha Makuyu wilayani Mvomero,Jafari Mohamed,akizungumza wakati wa zoezi hilo la kupanda miti,amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika suala zima la upandaji wa miti kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo makazi yao ili kupambana na uharibifu wa mazingira.
Mwisho.
0 Comments