Header Ads Widget

MIAKA 60 YA MUUNGANO TASAF YALIPA BILIONI 824.4 KAYA MASKINI

Na Hamida Ramadhani Matukio Daima app Dodoma

KATIKA kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mpango wa kunisuru Kaya Masikini TASAF umekuwa na manufaa makubwa ambapo katika eneo la Uhawilishaji wa Ruzuku kwa Walengwa kiasi cha Shilingi  bilioni 824.4 kililipwa kwa Kaya Maskini 1,321,098 Tanzania Bara na Shilingi  bilioni 41.2 ililipwa kwa Kaya Maskini 50,818 Zanzibar ili kuziwezesha kumudu gharama za msingi za maisha na kupeleka watoto wao shule na kliniki.


Akiongea na waandishi wa habari leo jijini hapa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma  na Utawala Bora George Simbachawene kuhusu mafanikio ya Miami 60 ya Utumishi wa umma na Utawala Bora


Amesema TASAF iliandaa Mpango wa Miradi ya kutoa Ajira ya muda kwa Kaya za Walengwa ili kuongeza kipato kwa kushiriki kufanya kazi katika miradi iliyoibuliwa na jamii kwa kulipwa ujira ambapo Tanzania Bara miradi 27,161 ya muda iliibuliwa na kutekelezwa katika Vijiji/Mitaa 9,891 huku Walengwa 626,620 walipata ajira ya muda na kulipwa kiasi cha shilingi bilioni 110.4, wakati Unguja na Pemba katika shehia 244 miradi 702 iliibuliwa na kutekelezwa na Walengwa 35,754 ambao walilipwa ujira wa kiasi cha shilingi bilioni 13.2.



Amesema serikali ya Awamu ya Sita na awamu zilizopita zinazoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zote zimekuwa na malengo kabambe ya kupunguza na kuondoa umaskini wa kipato ili nchi iwe na maendeleo tunayoyatarajia.


Waziri huyo amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati ya Serikali katika kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii.


Amesema,Madhumuni ya kuanzishwa kwake ilikuwa pia ni kusaidiana na taasisi zingine za Serikali ili kupambana na umaskini wa wananchi wake katika maeneo ya Vijijini na pembezoni mwa Miji ambapo TASAF imetekelezwa katika Awamu Tatu tangu kuanzishwa kwake hadi sasa. 

Ameeleza TASAF imekuwa ikitekelezwa kwa awamu tangu kuanzishwa kwake Awamu ya Kwanza ya TASAF ilianza mwaka 2000  2005 na ilijumuisha maeneo ya utekelezaji 42 ambapo 40 ni ya Tanzania Bara na mawili (2) ya Zanzibar (Unguja na Pemba). 


"Jumla ya miradi 1,704 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 72 ilitekelezwa kupitia mpango huu wa TASAF I. Awamu hii ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii katika sekta mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, miundombinu na afya, ".


Na kuongeza"Awamu ya Pili ya TASAF ilianza utekelezaji mwaka 2005 hadi 2013 Ili kuendeleza mafaniko yaliyopatikana katika Awamu ya Kwanza kwenye maeneo mengine ambapo Awamu hii ilitekelezwa katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. 


Amesema Jumla ya miradi 12,347 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 430 ilitekelezwa wakati wa Awamu hii ya Pili ya TASAF (TASAF II).


" Katika kipindi cha utekelezaji wa TASAF Awamu ya Kwanza na ya Pili, wananchi walishiriki vyema kutekeleza miradi mbali mbali iliyoboresha upatikanaji wa huduma za jamii ,Mbali na miradi ya kuboresha miundombinu kama vile barabara, maji, masoko, huduma za afya, elimu, ustawi wa jamii na mazingira, wananchi katika makundi mbali mbali walitekeleza miradi ya kuongeza kipato ambayo iliwasaidia kukabiliana na umaskini, " Amesema 


Aidha amesema awamu ya Tatu ilianza kutekelezwa Agosti, 2012. Awamu hii inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kwa lengo la kuziwezesha kaya masikini kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu.


"Utekelezaji wa Mpango huu umegawanyika katika vipindi viwili vya miaka mitano kwa kila kipindi, Kipindi cha Kwanza kilianza Mwaka 2012 na kukamilika Mwaka 2019 Kipindi cha Pili kilianza kutekelezwa Desemba 2019 baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa Kipindi cha Kwanza na utekelezaji utakamilika September 2025,"


Hata hivyo amesema Moja kati ya shughuli kuu za Mpango wa TASAF awamu ya tatu kipindi cha kwanza ilikuwa ni utoaji wa Ruzuku kwa Kaya za Walengwa. Katika Kipindi cha Kwanza kiasi cha shilingi billion 968.7 zilikuwa zimehawilishwa kwa kaya za walengwa zipatazo 1,118,752 katika vijiji, mitaa na shehia 9,831. 


Hali kadhalika katika Kipindi cha Pili hadi kufikia Juni 2023 kiasi cha shilingi bilioni 696.7 zimehawilishwa kwa kaya za walengwa zipatazo 1,371,916 katika vijiji, mitaa na shehia 17,260. 


Aidha, Mpango umekuwa ukitekeleza Miradi ya Ajira ya Muda ambapo unatoa ajira ya muda kwa kaya ya mlengwa ili kuongeza kipato cha kaya na kuiwezesha jamii kupata raslimali itakayochochea maendeleo ya sehemu husika. Jumla ya miradi 17,421 imetekelezwa ambapo kaya zipatazo 676,610 zilishiriki kufanya kazi katika sekta mbalimbali za kutoa huduma kwa jamii kama afya, elimu na maji na kulipwa ujira. 


Miradi mingine ililenga kutatua changamoto zinazohusu mawasiliano, usafirishaji na utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji. 


Vile vile Mpango katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ilitekeleza afua ya Kukuza Uchumi wa Kaya ambayo inahusiana na uhamasishaji wa uundaji wa vikundi vya kuweka akiba na kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji mali. Vikundi 46,569 vyenye wanachama 627,508 vilianzishwa.


Pia amesema TASAF Awamu ya Tatu kwa sasa inatekeleza Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambacho kinafanyika katika Mamlaka ya maeneo ya utekelezaji 186 ya Tanzania Bara na Zanzibar yakihusisha Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji ya Tanzania Bara na Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar.


" Lengo ni kuziwezesha Kaya za Walengwa kutumia fursa za kuongeza kipato, kutumia huduma za Kijamii na Kiuchumi na kuwekeza katika kujenga na kuendeleza watoto wao ambao ni rasilimaliwatu, ".


Sambamba na hayo Kumekuwa na mpango wa kuendeleza na kuboresha miundombinu ya huduma za jamii ambapo miradi 77 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya Elimu, Afya na Maji  yenye thamani ya shilingi bilioni 3.6 imetekelezwa katika Halmashauri 50 za Tanzania Bara wakati miradi 20 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.9 imetekelezwa Pemba na Unguja kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya huduma za jamii katika maeneo husika.

"Kupitia mpango huu, Serikali ya Awamu ya Sita imekuza uchumi wa Kaya Maskini kwa kuhamasisha Walengwa kuunda vikundi vya kuweka akiba, kukopeshana na kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji mali ili kuinua kipato cha Kaya. ,"


Na kuongeza " Tanzania Bara vikundi vya kuweka akiba 26,842 vyenye wanachama 358,846 viliundwa katika Mamlaka za Maeneo ya utekelezaji na viliweza kuweka akiba ya kiasi cha Shilingi bilioni 6.3, kati ya fedha hizo kiasi cha bilioni 2.7 kilitolewa kama mikopo kwa wanachama wake, " 


Kwa upande wa Unguja na Pemba, jumla ya vikundi 3,211 vyenye wanachama 45,948 vimeundwa na vimeweza kukusanya jumla ya akiba ya shilingi bilioni 1.6 kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 365.9 kilikopeshwa kwa wanachama.


Amesema hadi kufikia Machi, 2024, Walengwa wamepewa mafunzo ya stadi za msingi za kuendesha shughuli za kiuchumi kwa pande zote za Muungano ikiwa Tanzania Bara walengwa 27,964 kutoka Halmashauri 33 walipatiwa mafunzo na Ruzuku ya Uzalishaji ya kiasi cha Shilingi bilioni 8.6 na Unguja na Pemba Walengwa 23,399  na walipewa  Ruzuku ya kiasi cha Shilingi bilioni 8.9.


Amesema Fedha hizo ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yao ya kuzalisha na kuongeza kipato  cha Kaya. 


"Ili kupima matokeo ya Utekelezaji Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulifanyiwa tathmini ambayo ilionesha kuwa Mpango umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha maisha ya walengwa na kupunguza umaskini, "


Na kuongeza "Baadhi ya matokeo ni kama vile Kupunguza kiwango cha umaskini uliokithiri kwa asilimia 8 kwa kuongeza uwezo wa kaya kumudu gharama za mahitaji ya msingi ya kaya kwa asilimia 10;.Kuongezeka kwa idadi ya walengwa wanaoshiriki katika shughuli za kilimo na ongezeko la matumizi ya pembejeo ambazo zinaongeza tija kwenye uzalishaji; Ongezeko la uandikishwaji na mahudhurio shuleni kwa watoto kutoka kaya maskini kwa asilimia 6; Ongezeko la matumizi ya huduma za afya miongoni mwa kaya za walengwa na kuongezeka kwa mahudhurio kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa watoto wenye umri kati ya miezi 0-24 kutoka kaya maskini; Kuongezeka kwa akiba na rasilimali za kaya ambazo zinawezesha kaya kujikinga na majanga yanapotokea; Kuboresha makazi ya Kaya kwa kujenga nyumba bora kwa kutumia matofali ya kuchoma au saruji na kupaua kwa mbao na kuzifunika kwa bati, " Amesema


Hata hivyo Tathmini hiyo ilifanywa na taasisi bobezi katika eneo hilo ambazo ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Tanzania Bara na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali - Zanzibar


Pia amesema katika suala la ushirikiano ndani ya ofisi hiyo linajitokeza katika kuzuia na kupambana na rushwa kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).


Katika miaka 60 ya Muungano, kwa kuzingatia awamu zote zilizopita na hii inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa ili wananchi waweze kupata huduma bora.

 

Amesema kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kutambua kuwa Skauti ni suala la Muungano, TAKUKURU kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ziumeunda timu ya uratibu ya kitaifa yenye Wajumbe kutoka Chama cha Skauti Tanzania (CST), ZAECA na TAKUKURU ili kuimarisha ushirikiano katika jitihada za kupambana na rushwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


"Ushirikiano huu ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa kwa kuwa Skauti wapo katika kundi la vijana na ni Jeshi kubwa ambalo tumeshuhudia likitoa mchango chanya katika matukio mbalimbali ya kijamii na kitaifa, "


Na kuongeza "Vijana hawa, kupitia ushirikiano huo, wameelimishwa kuhusu madhara na jinsi ya kuzuia na kupambana na rushwa ili wakaelimishe vijana wenzao na jamii kwa jumla katika maeneo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS